Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano na Serikali ya China katika nyanja mbalimbali kupitia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, nishati na miundombinu.

Ameyasema hayo mapema hii leo alipokutana na  Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli kwenye nyumbani kwake, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Majaliwa amesema ushirikiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria, hivyo ameihakikishia Serikali ya China kwamba utaendelezwa kwa manufaa ya wananchi wa Mataifa yote mawili.

Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini China kuja kuwekeza  katika sekta mbalimbali nchini zikiwemo za miundombinu, viwanda, kilimo na nishati.

“Tanzania iko tayari kupokea kampuni zaidi za China kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini.Tupo tayari kupokea viwanda kati ya 200 hadi 700 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo,” amesema Majaliwa.

Kwa upande wake Mheshimiwa Wang Yi amepongeza utendaji kazi wa Rais Dk. Magufuli pamoja na viongozi wengine hususan katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi na tayari matunda yameanza kuonekana.

 

Video: Machinga Kariakoo wampongeza JPM, wataja elimu bure kuwanufaisha
Wachimbaji wadogo wadogo wa madini kuanza kunufaika