Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kudhibiti matumizi ili kuendana na mpango na bajeti ya 2022/2023, ambapo ametumia fursa hiyo kuielekeza Wizara na taasisi zote za Serikali kuzingatia vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/2024 katika maandalizi ya bajeti za mafungu husika.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma na kuzielekeza Halmashauri zote nchini zenye mapato yasiyolindwa chini ya shilingi bilioni mbili (Kundi C), zihakikishe zinatenga kiasi kisichopungua asilimia 20 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikijumuisha asilimia 10 ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Amewataka Wakuu wote wa Mikoa wahakikishe wanasimamia kwa karibu miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao ili miradi hiyo iweze kuakisi thamani ya matumizi ya fedha za umma.
Aidha, Majaliwa pia amewaelekeza Maafisa Masuuli wote wazingatie kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2023/2024 ikiwa ni pamoja na kuzingatia kikamilifu Sheria ya Bajeti (SURA 439) na Kanuni zake.