Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itamchukulia hatua mzazi au mtu yeyote atakayemzuia mwanafunzi kupata haki yake ya elimu, na kuwataka wazazi wote wenye wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza, kuhakikisha watoto hao wanaripoti kwenye shule walizopangiwa mara moja.

Majaliwa ameyasema hayo hii leo Februari 10, 2023 wakati akiahirisha Mkutano wa 10 wa Bunge la 12, Bungeni Jijini Dodoma na kutumia fursa hio kuziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo bado hazijakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kuhakikisha vyumba hivyo vinakamilika.

Amesema, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilitoa shilingi bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 8,000 vya madarasa katika shule za sekondari ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Hadi kufikia Februari 3, 2023 vyumba vya madarasa 7,874 sawa na asilimia 98.43 vimekamilika na vyumba vya madarasa 126 sawa na asilimia 1.57 vipo katika hatua mbalimbali za umaliziaji na ameongeza kuwa, “ukamilishaji wa ujenzi wa madarasa ya sekondari umewezesha wanafunzi wote 1,076,037 waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2022 kupata fursa ya kupangiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwezi Januari 2023 kwenye shule za Serikali kwa awamu moja pekee.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa, “Mafanikio haya ni kielelezo tosha cha umakini, uzalendo, maono na kazi iliyotukuka inayotekelezwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulinda maslahi na kujenga mustakabali mzuri wa Taifa letu.”

Wanafunzi wakisubiri usafiri kwenda Shule.

Akizungumzia kuhusu uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza na awali, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kufanya vizuri ambapo hadi kufikia tarehe 03 Februari, 2023 wanafunzi 1,363,320 wa darasa la awali wameandikishwa wakiwemo wenye mahitaji maalum 2,944 sawa na asilimia 100.18 ya lengo la kuandikisha wanafunzi 1,360,737.

Aidha, amefafanua kuwa, katika kipindi hicho wanafunzi 1,657,533 wakiwemo wenye mahitaji maalum 3,825 waliandikishwa kwa ajili ya darasa la kwanza sawa na asilimia 101.29 ya wanafunzi 1,633,659 waliotarajiwa kuandikishwa.

Tetemeko Syria, Uturuki: Vifo vyapanda tena sasa ni watu 21,000
Maelfu wajitokeza kuasili kichanga kilicho okolewa kwenye kifusi