Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema mtu yeyote atakayekutwa na hatia ya kuvunja sheria kwa kuvamia na kuharibu mazingira ya msitu wa Mfili ambao ndiyo chanzo pekee cha maji cha Wilayani Nkasi atatozwa faini ya sh. milioni 70 pamoja na kifungo miaka saba jela.

Aidha Katika kuhakikisha hatua zinachukuliwa Waziri Mkuu amemkabidhi mkuu wa wilaya ya Nkasi, Said Mtanda kitabu cha sheria kitachomuongoza katika kuwachukulia hatua wale  wote watakaobainika kufanya  uharibifu katika chanzo hicho cha maji.

Mh.Majaliwa ametoa kauli hiyo  wakati akizungumza na wananchi wa mji Mdogo wa Namanyere katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Sabasaba.

“Mkuu wa wilaya akishindwa kuwachukulia hatua za kuwaondoa wananchi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu wote waliovamia maeneo ya hifadhi za misitu na kuanzisha makazi au kufanya shughuli za kijamii naye atakuwa jipu,” alisema.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa maeneo mengi nchini yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji baada ya wananchi kuvamia katika vyanzo vya maji na kufanya shughuli za kibinadamu hivyo kusababisha vyanzo vingi kukauka.

“Serikali haitakubali kuona mtu anaharibu chanzo cha maji. Wananchi mnatakiwa kuwa walinzi wa maeneo hayo na atakayekutwa anachunga mifugo, analima, kukata nyasi au kufanya shughuli zozote za kijamii ndani ya maeneo hayo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Awali Mh.Majaliwa alikagua mradi wa upanuzi wa bwawa la maji Mfili ambalo mwanzo lilikuwa na ujazo wa lita 1,500 ambapo litakapokamilika litakuwa na ujazo wa lija 248,067 hivyo kuwezesha wakazi 82,689 kunufaika.

Akizungumza kwenye eneo la mradi mara baada ya Waziri Mkuu kuwasili, Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo alisema hadi kukamilika mradi huo unatarajiwa kugharimu sh trilioni 1.011 ambapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji imetoa sh. milioni 500 na Ofisi ya Rais TAMISEMI itatoa sh. milioni 500.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi huo alisema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu  umeme pamoja na mitambo ya kusukuma maji kwa kutumia nishati ya umeme, ambapo aliiomba Serikali kuipatia halmashauri hiyo sh. milioni 222.576 ikiwa ni gharama za kupeleka umeme kwenye eneo la mradi na kununua mitambo.

Mbali na kutembelea mradi wa upanuzi wa bwawa, pia Waziri Mkuu alitembelea hospitali teule ya wilaya ya Nkasi na kuzindua wodi mpya yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 72 kwa wakati mmoja.

Majaliwa;Watumishi Wataokula Hela Za CHF Wafukuzwe Kazi, Washitakiwe
Serikali haijazuia Taifa kuwa na vyama vya siasa ila haijaviruhusu kuvuruga amani - Waziri Mkuu