Na Lilian Mahena
Wahenga walisema tembea uone, basi leo katika matembezi yangu jijini Dar es salaam kwenda kuangalia maonyesho ya kimataifa ya biashara maarufu kama ‘Sabasaba’, jicho langu likaangukia kwenye fursa nzuri ya ujasiriamali.
Watu mbalimbali wamejitokeza kwenda kuangalia maonesho hayo jijini Dar es Salaam, ambayo yamekuwa chachu ya ukuaji wa biashara ndogo ndogo zinazotoa fursa ya ukuaji wa viwanda nchini.
Moja ya biashara ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa watu wengi ambayo jicho langu lilivutika kwa kasi zaidi ni ile ya ufugaji wa samaki kwa njia ya matanki inayopatikana katika banda la Jeshi la Kujenga Taifa JKT.
- Utafiti WHO: Mtindo huu wa kufanya mapenzi unawapoteza mamilioni duniani
- Trump uso kwa uso na Putin Ujerumani, kushona majeraha ya nchi zao
Kwa bahati nzuri, nilipata maelezo pia kutoka kwa wataalam wa ufugaji huo uliowawaacha mdomo wazi watu kwa muda, kwakuwa ni fursa kubwa unayoweza kuibadili kuwa utajiri nje ya nyumba yako.
Samaki wanaofugwa kwenye matanki ni aina ya sato ambao baada ya miezi minne wanakuwa na gram 350 mpaka 400. Ilikuweza kufikisha kiasi hicho samaki wanatumia gram 250 mpaka 300 ya chakula ambayo ni sawa na shilingi laki nne.
Ufugaji huo wa samaki unahitaji mtaji wa shilingi milioni tatu tu ambayo inajumuisha kupata matanki manne yenye uwezo wa kuweka samaki 100 kila tanki. Pia, mashine ya kuhifadhia umeme ukikatika (Back up) ambapo umeme unaotumika kwa siku ni ‘unit moja’ tu na invertor ili kupeleka hewa ya oksijeni kwa samaki.
Ausilyo Kisinini, mmoja wa wabunifu wa utaalamu huo wa ufugaji samaki amesema yeye na wenzake ambao ni Zena James, Grace Kigae na Nusura Jongo chini ya uongozi wa Luteni Lyakurwa wamebuni njia hiyo ili kuendana na kauli mbiu ya Rais John Magufuli ya ukuzaji wa biashara kwa maendeleo ya viwanda vidogo vidogo .
Aidha, aliongeza kuwa wazo hilo walilipata walipokwenda nchini Afrika ya Kusini kwa ajili ya kufanya utafiti juu ya ufugaji wa samaki kama moja ya somo wakiwepo jeshini. Alisema waligundua kuwa wenzetu (Afrika Kusini) wanatumia maturubai na mabomba. Hivyo, wao wakaja na ubunifu wao tofauti kidogo.
Ufugaji huo wa samaki utarahisisha sana upatikanaji wa samaki na hivyo kupelekea familia nyingi kuweza kupata kitoweo hicho kwa bei rahisi na hasa kufanya ufugaji wa samaki kuwa rahisi kama ufugaji wa kuku kwani kila mmoja kuwa na uwezo wakuweka matanki hayo nyumbani kwake na kuwahudumia samaki kirahisi.
Leo ni sikukuu ya Sabasaba, tafadhali tembelea eneo la maonesho ya sabasaba kujionea fursa, kuona ni kuamini na kutembea sehemu yenye fursa ni kuukaribia utajiri uliombele yako.
Kwa bahati nzuri, kutokana na wito wa Rais John Magufuli, maonesho hayo mwaka huu yataongezwa wiki moja zaidi.