Kwa mujibu wa tafiti, Watoto njiti Tanzania wanapoteza maisha wakiwa chini ya miaka mitano ambapo pia takwimu zinaonesha nchini Tanzania asilimia 17 ya watoto huzaliwa kabla ya muda wa mimba kukomaa na Watoto hao huwa katika hatari zaidi ya kupoteza maisha.

Hii hutokana na sababu mbalimbali zikiwemo watoto hao kushindwa kupumua, kupoteza joto la mwili kwa haraka, kupata uambukizo wa bakteria, kushindwa kunyonya na kupata manjano, hivyo ni wazi kuwa huwa wanahitaji huduma maalum.

Upatikanaji wa huduma bora ni suala muhimu linalowezesha utambuzi na udhibiti wa matatizo wakati wa ujauzito na uhakiki wa hesabu sahihi tangu mimba ikiwa changa kupitia uchunguzi wa kitabibu kwani mama anapozaa kabla ya wakati, hupelekea mtoto kuwa Njiti, kwakutofikisha muda wake wa kuzaliwa na mwili wake kutokomaa.

Kwa mujibu wa jarida la Afya la Lancet, inakadiriwa kuwa Watoto milioni 13.4 njiti (wanaozaliwa kabla ya wiki 37 za ujauzito), walizaliwa mwaka 2020 idadi ambayo ni takriban mtoto 1 kati ya 10 na wengi wa watoto hao ni kutoka Ukanda wa jangwa la Sahara na Asia ya Kusini.

Mhudumu wa Afya akimuweka mtoto mchanga eneo maalumu lenye joto lililopimwa (incubator), ili kuboresha uwezekano wa kuishi. Picha ya Irin /Sean Kimmons.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO, idara ya masuala ya Watoto Wachanga, Watoto, Afya za Barubaru na Wazee, Dkt. Anshu Banerjee aliwahi kusema kwamba kitendo cha mama kuzaa kabla ya muda, ni sababu kubwa ya vifo vya Watoto wachanga na kwamba suala hilo linapaswa kushughulikiwa kwa udharura.

Watoto wanaozaliwa njiti huhifadhiwa kwenye kifaa special (incubator), kinachowapa joto la kutosha kama alilokuwa analipata kwa mama tumboni, lakini kuna njia nyingine inaitwa Kangaroo ambapo mtoto hubebwa kifuani kwa mama yake au baba yake akiwa hana nguo, ila atavishwa soksi na kofia na atafunikwa ili apate joto la kutosha na ni njia moja wapo ya kumpa joto.

Aina za watoto njiti.

Watoto njiti wanakuwa wanatofutiana umri, kuna wale wanao zaliwa wakiwa na wiki 28 na kuna wa wiki 28 -32 huku baadhi ya watoto hao wanaozaliwa kati ya wiki hizi wakiwa wanapata tabu kwenye mfumo wa hewa na (mapafu), ambapo kundi la mwisho huzaliwa wakiwa na wiki 32-37. Njiti alie zaliwa kabla ya wiki 37.

Sababu za mama kuzaa mtoto njiti.

Hatari za afya ya uzazi, kama vile mimba za utotoni, maambukizi, lishe duni, na hali ya kutokwa na damu wakati wa ujauzito ni sababu zinazo husishwa na mama mjamzito kujifungua mtoto njiti ni jambo mojawapo lakini pia matumizi ya Pombe au dawa la kulevya vyote hivyo huchangia mama kuzaa mtoto njiti.

Uchukuajiwa Vipimo wakati wa ujauzito.

Vilevile kuna suala la upungufu wa damu mwilini, uzito mkubwa kwa mama kipindi cha ujauzito, uvutaji wa sigara au bangi, Mama kuwa na ugonjwa kama kisukari, pressure, infections au kifafa cha uzazi, matatizo ya mama kwenye cervix ambayo hupelekea kushindwa kujifunga na kujikaza kubeba mtoto na kondo (placenta), inapokuwa na tatizo.

Sababu nyingine ni Mama kushika mimba haraka baada ya kujifungua mtoto mwingine, Mama kuwa na mimba ya mapacha chupa kupasuka kabla ya muda wake (mama atabidi azae kabla ya mda Wake), stress na kushika mimba chini ya miaka 17 au zaidi ya miaka 35 pia kuna hatari ya kuzaa mtoto njiti.

Lakini pia kuna suala la Mama kutohudhuria Klinik vizuri na kukosa baadhi ya kipimo, supplements kama za prenatals vitamins au foilic acid zinazomsaidia yeye na mtoto kipindi chote cha mimba anatakiwa atumie na lishe mbaya ni chanzo cha kuzaa mtoto njiti.

Dalili ya mama mjamzito anaetaka kuzaa mtoto njiti.

Unapotaka kuepuka kuzaa mtoto njiti, lazima mama anatakiwa ajue dalili ni zipi na ukishaziona inakubidi uwahi hospital, Maumivu ya mgongo-utasikia mgongo unauma sana maeneo ya chini maumivu yakuja na kuondoka, maumivu ukeni kunavuta na kuachia kila baada ya dakika 10, kutokwa maji maji ukeni kwa wingi.

Watoto Njiti katika hospitali ya Al Shifa iliyopo Gaza.

Dalili nyingine ni kutokwa na damu inaweza kuwa nyingi au kidogo ukeni, kuhara, kutapika, maumivu chini ya kitovu, mtoto kukusukuma kuja chini (kuhisi pressure kuja chini), kutokucheza kwa mtoto (mama unatakiwa ufatilie mtoto mapigo yake tumboni ukisikia yupo kimya jaribu kunywa maji, uji, chai au kula chakula atacheza ukaona kimya kinazidi kwa mda mrefu wahi hospitali).

  • Hatari za Mtoto njiti baada ya kuzaliwa.

Baadhi ya watoto njiti wanakuwa na hatari ya Kushindwa kupumua na huwa na hatari ya kupata athari kwenye ubongo hali itakayopelekea milango ya fahamu na organs kuathirika, sambamba na ukuaji mbaya (afya isiyo nzuri), ingawa sio wote wanaokuwa na afya dhoofu baada ya kukua.

Wengine huwezi jua kama walizaliwa njiti kutokana na afya bora walizo nazo, hivyo mama hutakiwa aanze kliniki mapema, ili upewe mafunzo ya kulea mimba pamoja na vipimo muhimu na ikumbukwe pia asilimia 65 ya watoto njiti waliozaliwa mwaka 2020 walitokea Kusini mwa jangwa la Sahara, na Asia Kusini na walikuwa asilimia 13.

Taarifa ya WHO pia ilibainisha kuwa mbali na suala la watoto kupoteza maisha, watoto njiti wanakabiliwa na ukuaji wenye changamoto, ikiwemo kupata magonjwa makubwa, ulemavu na ukuaji kwa kuchelewa na hata wakiwa watu wazima wanaweza kupata magonjwa sugu, kama kisurari na magonjwa ya moto.

Wanasayansi wa Marekani wanasema wamebuni tumbo bandia, ambalo litatumika kuhifadhia watoto wanaozaliwa kabla ya muda (Njiti).

Utafiti unaonesha kuwa, suala la watoto njiti sio la nchi tajiri au masikini, bali wajawazito wote wanaweza kuathirika katika kila kona ya dunia huku takwimu zikionesha zaidi kuwepo kwa idadi kubwa ya watoto njiti katika nchi tajiri Ugiriki yenye asilimia 11.6 na Marekani yenye asilimia 10.

  • Utokomezaji Watoto Njiti Tanzania.

Mapema hivi katibuni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko aliwataka wadau wa masuala ya Afya ya Watoto nchini, kushirikiana kutokomeza tatizo la watoto waliozaliwa kabla ya wakati (watoto Njiti).

Wito huo, aliutoa wakati wa hafla ya kusherehekea mafanikio ya Ajenda ya Mtoto Njiti (2021) iliyofanyika jijini Dodoma na kusema takribani watoto milioni 15 duniani huzaliwa Njiti huku nchi za Bara la Asia na Afrika hasa kusini mwa jangwa la Sahara, zikiongoza kwa asilimia 80 ya vifo vya watoto hao.

Alisema, “inakadiriwa kila mwaka watoto 336,000 huzaliwa njiti nchini Tanzania na zaidi ya watoto 11,500 hupoteza maisha kutokana na changamoto za kuzaliwa njiti. Ni kweli kwamba kiwango cha kuzaliwa kwa watoto njiti hapa nchini kimekuwa kikiongezeka. Hatuna budi kuzidisha mapambano na ningefurahi siku moja itokee taarifa kuwa hakuna vifo vya watoto njiti nchini kwetu.”

Mimba za utotoni pia zinatajwa kama sababu mojawapo inayopelekea kuzaa mtoto njiti.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Ridhwan Kikwete naye alisema akipata nafasi ya kuwasilisha hoja kuhusu sheria ya utumishi na likizo ya uzazi atashauri likizo ya uzazi ifikie miezi sita, ili watoto njiti wapate malezi stahiki.

  • Nini kifanyike.

Ni wazi kuwa kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha anashiriki kwa sehemu yake kupambana na hatari au vyanzo vinavyopelekea upatikanaji wa mtoto njiti, kuhakikisha matibabu kwa mama akiwa mjamzito, ambayo yanaweza kuzuia matatizo ya kupumua.

Pia hili linaweza kusaidia kupunguza hatari za kiafya kwa watoto waliozaliwa njiti pamoja na matibabu ya kuchelewesha uchungu wa kujifungua, sote tukishikamana tunaweza kuokoa na kuwafanya watoto waliozaliwa njiti waweze kukua vyema na kuishi.

Serikali pia iangalie upya sheria ya likizo ya uzazi aweze kukaa na mtoto huyu kwa muda wa kutosha, kwani baba anapata likizo ya siku tatu na mama likizo ya miezi mitatu, lakini mtoto njiti mpaka afike miezi 6 kashatumia miezi mitatu.

Ukumbatiaji wa watoto njiti ni njia mojawapo inayoweza kuleta ufanisi wa ukuaji mzuri wa mtoto aliyezaliwa Njiti.

Lakini pia kuangalia namna ya kubeba gharama kupitia bima ya afya, kwa hali ya sasa mama aliyepata mtoto njiti analazimika kubeba gharama za matunzo ya huyu mtoto hasa pale panapohitajika huduma maalum kama za dawa za kukomaza mapafu na dawa hizo ni gharama sana na dozi moja inauzwa kati ya shilingi laki 5 hadi 6 na mtoto anaweza kuhitaji hadi dozi tatu ili aweze kuwa sawa, kununua mipira ya kulishia iwapo mtoto hawezi kunyonya maziwa ya mama yake.

Watoto wengine huhitaji maziwa bandia ambayo ni ghali mno hivyo, jamii ielimishwe kuanzia Shuleni kwa kushirikiana na Wizara, ili kuanzisha mtaala wa kusaidia kuingia elimu ya watoto njiti kwenye mtaala wa Tanzania.

Hii itasaidia Wananchi wenye uelewa wa jinsi ya kujikinga au kujipa msaada ili wasipate mtoto njiti na hata akitokea wasione kuwa si riziki au mtoto huyu hatoishi kwani Watoto njiti wanaishi wakiwapatiwa maisha bora.

Mchakato wa Kocha Simba SC wafikia 90%
Mashabiki, Wanachama Simba SC watulizwa