Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Phillip Mpango amekemea tabia ya wizi wa maji inayofanywa na baadhi ya watu nchini, wakiwemo wawekezaji wakubwa.
Dkt. Mpango ameyasema hayo hii leo Januari 19, 2023 mjini Shinyanga wakati akiweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria utakaohudumia Tinde na Shelui na unaotarajia kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 24.4.
Amesema, mamlaka za maji zinatakiwa kuacha kutoza faini ndogo kwa wanaokutwa na hatia za wizi wa maji na kuvitaka vyombo vyote husika kufuatilia na kuwachukulia hatua wezi wote pamoja na wale wanaochepusha maji kutoka kwenye mito bila vibali halali.
Amesema, maji ni miongoni mwa Sekta za kipaumbele katika mkakati wa kukuza Uchumi wa Viwanda na kupambana na umaskini na kwamba kuboresha huduma hiyo kutapunguza muda wa kutafuta na kuchota maji, ili kuwawezesha Wananchi kufanya kazi za kimaendeleo.