Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kama mwanamke na kiongozi katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, anajivunia kuona Serikali ikiwa imefanya jitihada mbalimbali katika kumwezesha mwanamke katika maendeleo kwa jumla.
Kupitia ujumbe wake wa siku ya leo, makamu wa rais amesema, serikali imeendelea kuhakikisha Sera ya elimu bure inayotekelezwa na serikali imetoa fursa kwa watoto wengi wa kike kuandikishwa shuleni pamoja na kuzihimiza taasisi za kifedha kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kuwawezesha wanawake wengi kunufaika na mikopo hiyo.
Aidha makamu wa Rais amesema, serikali yake itaendelea kuboresha huduma za kijamii kama vile kujengwa zahanati na vituo vya afya na usambazaji wa maji ili vimpunguzie mwanamke usumbufu na hivyo kumpa muda wa kutosha kufanya shughuli za maendeleo.
Amesema, usambazaji umeme vijijini kwa kiasi kikubwa umesaidia wanawake wengi kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato pamoja na kurasimisha vikoba pamoja na kuwashawishi wanawake wengi zaidi kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuweza kunufaika na mafao na mikopo itolewayo na taasisi hizo.
Mama Samia amesisitiza pia kuwa serikali imejipanga kuwezesha wanawake kupatiwa asilimia tano (5) ya mapato ya halmashauri na asilimia 30 ya zabuni za halmashauri kwa ajili ya wanawake wengi kufanya biashara na hatimaye kuwa na uhakika wa kipato.