Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Kenya, Eugene Wamalwa Viongozi wa vuguvugu la Azimio la Umoja-One akiwemo kinara Raila Odinga, Martha Karua, Kalonzo Musyoka (Wiper), na baadhi ya magavana, wameondolewa ulinzi na Serikal.
Wamalwa amefichua hayo na kusema kitendo hicho kinasikitisha kwani Serikali imechukua hatua hiyo wakati ni inafahamika bayana kwamba Odinga na Kalonzo ambao waliwahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mtawalia, wanahitajika kuwa na walinzi kwa mujibu wa Katiba.
Amesema, “Odinga alikuwa Waziri Mkuu wa Pili naye Musyoka alikuwa Makamu wa Rais wa 10 na hivyo ni wajibu wa serikali kuwapa ulinzi. Isitoshe, hatua hii ya kuondoa walinzi inajiri wakati kundi linaloogopewa la polisi waangamizaji la OSU likiongozwa na Zachary Kariuki limefufuliwa,” amesema Wamalwa.
Aidha, ameongeza kwamba tayari athari za Serikali kutojali maisha ya Wakenya imejidhihirisha wazi na kutoa picha ya kile kinachoendelea akidai kuna mashambulio yaliyopangwa na yanayoendelea katika eneo la Sondu na yatatekelezwa katika kaunti kadhaa, huku akitoa wito kwa Polisi wajiepushe dhidi ya kukubali kutumiwa vibaya na viongozi wa Kenya Kwanza.