Rais wa chama cha soka nchini Zambia (FAZ) Andrew Kamanga, amependekeza kikosi cha timu ya taifa ya vijana cha nchi hiyo chini ya umri wa miaka 20, kituzwe ili kiweze kupewa jukumu la kuwa timu ya taifa ya wakubwa kwa siku za usoni.

Kikosi cha vijana cha Zambia chini ya umri wa miaka 20, kiliondolewa kwenye fainali za kombe la dunia hatua ya robo fainali kwa kufungwa na Italia mabao matatu kwa mawili siku ya jumatatu huko Korea kusini.

Kamanga amesema anaamini ushujaa na kujiamini kwa wachezaji wa kikosi hicho kumetoa mwanga kwa kila mpenda soka nchini humo, kuamini siku za usoni kutakua na kikosi kikali ambacho kitatikisa barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Hata hivyo kiongozi huyo ambaye alingia madarakani mwezi March mwaka jana, amesema vijana hao watakabiliwa na jukumu la kucheza michezo yakuwania kufuzu michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020 itakayofanyika mjini Tokyo nchini Japan.

Amesema endapo kitafanikiwa kufaulu mtihani huo, kitaendelea kupata uzoefu wa kutosha wa mapambano ya kimataifa kabla ya kuchukua jukumu lingine la kuhakikisha wanafuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2021.

Asilimia kubwa ya wachezaji wanaounda kikosi cha timu ya taifa ya Zambia chini ya umri wa miaka  20, walikua kwenye kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 17 kilichoshiriki fainali za Afrika kwa vijana za mwaka 2015 zilizochezwa nchini Niger.

Wakati huo huo kikosi Zambia kimewasili mjini Lusaka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kenneth Kaunda leo mchana kikitokea Korea kusini.

Rais wa Zambia Edgar Lungu, alitarajiwa kuwapokea vijana hao lakini majukumu ya kitaifa yalimzuia kufanya hivyo.

Kabla ya kuanza safari ya kuondoka Korea Kusini, Rais Lungu aliwatumia ujumbe na kuwaita Mashujaa waliokubaji kujitoa kwa ajili ya nchi yao.

Ndege ya kijeshi yapotea na watu 116
ACT Wamvua Uenyekiti Anna Mghwira, Washauri Uteuzi Ufuate Taratibu Hizi