Chama cha ACT-Wazalendo kimemvua uenyekiti wa chama hicho, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kufuatia uteuzi wake.

Uamuzi huo umetangazwa leo na Katibu Mkuu wa chama hicho, Samsoni Mwigamba alipofanya mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mwigamba alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubaini kuwa kutokana na uteuzi huo, Mghwira hawezi kufanya kazi ya uenyekiti wa chama hicho kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo wa chama amesifia uamuzi wa Rais John Magufuli kuwateua watu kutoka upande wa upinzani, lakini ameomba kamati ya uongozi kumshauri kuweka mfumo bora wa kufanya uteuzi kutoka upande wa upinzani ili kuepusha migongano.

“Kamati ya uongozi inamshauri rais kuweka mfumo bora wa kuazima watu kutoka vyama vingine kwa kuweka mashauliano ili kuepuka migongano ndani ya vyama,” alisema.

Alisema kuwa kamati ya uongozi imemteua Yeremia Kulwa Maganja kuwa kaimu M/kiti wa chama Taifa hadi uchaguzi mkuu 2018.

Jana, rais John Magufuli alimuapisha Mghwira kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro na kuahidi kuendelea kuwateua wapinzani kwa kadiri inavyofaa kwani anataka kufanya kazi bila kujali itikadi ya vyama.

Mama Mghwira aligombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu uliopita kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo.

Makinda Ya Zambia Yabebeshwa Majukumu
Gillingham Yamsajili Gabriel Zakuani