Hatma ya wachezaji wa Azam FC watakaobaki kukitumikia kikosi hicho msimu ujao ipo mikononi mwa makocha kutoka Hispania, ambao tayari wamerejea Dar es Salaam juzi wakitokea kwao kwa mapumziko.

Msemaji wa Azam FC, Jaffar Idd alisema tayari benchi la ufundi likiongozwa na kocha mkuu, Zeben Hernandez na msaidizi wake, Yeray Romero, kocha mkuu wa viungo, Jonas Garcia na msaidizi wake, Pablo Borges na kocha wa Makipa, Jose Garcia wamefika kuanza kazi rasmi wiki hii.

Alisema jopo hilo la makocha litaongezewa nguvu na makocha wengine wazawa waliokuwa na Azam FC msimu uliopita, kocha msaidizi Dennis Kitambi na wa makipa, Idd Abubakar.

Idd alisema kocha huyo mpya na jopo lake litakaa leo na uongozi wa klabu hiyo kuweka mikakati ya maandalizi yao.

“Makocha tayari wamekuja na leo watakutana na viongozi na baada ya hapo wataanza mazoezi na wachezaji wote pamoja na wale watakaokuja kufanya majaribio kuangalia ni wapi watakaobaki au kutemwa,” alisema.

Msemaji huyo alisema mazoezi ya kwanza ya timu yatahudhuriwa na wachezaji wote waliokuwemo msimu uliopita.

Pia, Alhamisi wataanza kuwapokea wachezaji wapya kwa ajili ya majaribio, ambapo hatma ya wale watakaochukuliwa itatokana na jinsi makocha hao watakavyowaona.

Alisema wanatarajia kumpokea daktari wa timu hiyo, Sergio Perez, kuanzia Julai 12 mwaka huu.

Alisema tayari wachezaji waliomaliza mikataba yao wameshakabidhiwa barua zao kwa ajili kutafuta timu kwingine. Miongoni mwao ni Didier Kavumbagu na Frank Domayo, ambao mikataba yao ilimalizika.

Naye, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema kuwa katika maandalizi yao wamejipanga kuwatafutia makocha hao mechi za kirafiki za kimataifa, endapo hakutakuwa na michuano ya Kombe la Kagame walilolitwaa mwaka jana

Roma ataja siku ya kuiachia Video na Audio ya ‘Kaa Tayari’… kuyapekua matukio ya JPM?
Joseph Omog Awaita Wachezaji Wote Mazoezini