Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza vita kali kwa watu wanaojihusisha na dawa za kulevya mkoani humo.

Akiongea leo jijini Dar es Salaam na viongozi wa serikali wa ngazi mbalimbali wa Mkoa huo, Makonda aliwataka viongozi wa ngazi za chini hususan Wenyeviti wa Mitaa kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kuwabaini watu wanaojishughulisha na dawa za kulevya.

Mkuu huyo wa Mkoa ameweka wazi kuwa hivi sasa haogopi kufa kwa kuwa tayari alimeshayafikia mafanikio aliyoyahitaji hivyo ni bora afe akipigania Taifa lake. Amewataka viongozi wenzake pia kutoogopa kufa kwakuwa lazima watakufa bali kinachoangaliwa ni sababu za kifo.

Amewataka wenyeviti wa mtaa ambao ndio wanaishi kwa karibu zaidi na wananchi waweze kuwasiliana moja kwa moja na wakuu wa wilaya pamoja na wakuu wa polisi kwa njia ya simu za mkononi ili kuwajulisha kuhusu vitendo vya kihalifu vinavyoendelea katika maeneo yao.

Katika kuhakikisha Jeshi la polisi linapata ari zaidi ya kufanya kazi ya kudhibiti uhalifu, Makonda amesisitiza kuwa atakuwa anatoa motisha ya shilingi milioni moja kwa polisi atakayeonekana kufanya vizuri zaidi.

“Polisi atakayefanya vizuri… mimi nitawapa shilingi milioni moja kila baada ya miezi mitatu kwa kuwashindanisha,” amesema Makonda.

Rais Magufuli ateua wakurugenzi wakuu wapya NSSF, TBC na RAHCO
P Square: Paul amuomba msamaha Peter, maneno yake ya kubembeleza yazaa hili