Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametangaza kuwakataa Mkurugenzi wa Jiji hilo na msaidizi wake baada ya kufanya uchunguzi na kubaini wamehusika katika ubadhirifu wa fedha na maamuzi yao kulikosesha jiji hilo zaidi ya shilingi bilioni 3.

Akiongea jana na waandishi wa habari jijini humo, Makonda alisema kuwa hataki kufanya kazi tena na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe na Kaimu wake, Sarah Yohana na na kwamba ameyawasilisha majina yao kwa mamlaka husika ya nidhamu kwa hatua zaidi.

UBUNGO1

Akielezea madudu aliyoyabaini, alisema kuwa watumishi hao waliruhusu Kampuni iliyopewa dhamana ya kukusanya tozo katika stendi ya Ubungo, kwa makusudi kutumia sheria ndogo ya  ukusanyaji mapato ya mwaka 2004 inayotaka kila basi kutozwa shilingi 4,000 wakati kuna sheria mpya ya mwaka 2009 inayotaka kila basi kutozwa shilingi 8,000.

Alisema kuwa makampuni hayo yaliendelea kusaini mkataba na kuidhinishwa Mkurugenzi huyo kwa kutumia sheria hiyo, hivyo kupoteza shilingi milioni 42 kwa mwezi.

“Cha kushangaza tumebaini kuwa bado kampuni inayokusanya mapato katika kituo cha Ubungo, inawasilisha mapato hayo kwa kutumia sheria ya mwaka 2004 yaani Shilingi milioni 42 badala ya Shilingi milioni 82 kwa mwezi,” alisema Makonda.

Alisema kuwa kamati maalum aliyoiunda kufanya uchunguzi ilibaini licha ya kuwa kampuni hiyo inayo sheria ya mwaka 2009, nyaraka zake zilizopo katika Halmashauri ya Jiji inaonesha kuwa inatumia sheria ya mwaka 2004 katika malipo.

Makonda pia aliorodhesha ukiukwaji wa sheria na mkataba unaofanywa na kampuni hiyo iliyopewa zabuni na jiji. Alisema kuwa Kampuni ya Tambaza inayosimamia makosa ya pikipiki na maegesho imekuwa ikitoza faini ya shilingi 80,000 wakati mkataba unawataka kuangalia dharura na kutoza shilingi 20,000 wanapokamata pikipiki.

Mkuu huyo wa mkoa ameeleza kuwa tayari amewasilisha mikataba husika katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini ili waweze kuifanyia kazi.

 

Lady Jay Dee aiongezea nguvu E-FM baada ya Gardner kuikacha
Mwakyembe awaonya Polisi wanapokamata watuhumiwa