Kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Hereos) Malale Hamsini Keya amezidi kuwa na wakati mgumu baada ya timu mbili za ligi kuu tofauti kumng’ang’ania.

Kocha huyo ameifundisha timu ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) kwa mafanikio makubwa ambapo msimu ulopita ilirejea kucheza ligi kuu soka Zanzibar na kufanikiwa kupata nafasi ya pili na msimu huu February 14 itacheza na timu ya Gabarone United ya Botswana katika mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika.

Msimu huu Malale ameiongoza JKU katika michezo 10 ya ligi kuu soka Zanzibar kanda ya Unguja na kufanikiwa kushinda michezo 9 na kwenda sare mchezo mmoja bila hata ya kupoteza.

Lakini michezo miwili iliopita JKU aliposhinda 4-2 dhidi ya KMKM na ule waliopigwa 1-0 na Miembeni yote hakuonekanwa katika benchi la ufundi la JKU siku hizo zote mbili.

Taarifa zikazagaa kuwa kocha huyo katimkia mkoani Mtwara kwenye klabu ya Ndanda FC inayokipiga ligi kuu soka Tanzania bara.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Malale alikataa kata kata alipoongea na Muandishi wa Habari hii kuwa hajaenda Ndanda FC, lakini cha ajabu Jumapili iliopita ya tarehe 31 mwezi wa January, alianza rasmi kibarua chake akiwa na Ndanda FC walipocheza na  Mgambo JKT, kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga kwenye muendelezo wa ligi kuu soka Tanzania bara ambapo walitoka sare bao moja kwa moja.

Lakini Juzi jioni ameripotiwa alikuwepo visiwani Zanzibar na jana asubuhi aliwafundisha wachezaji wa JKU mazoezi kwenye uwanja wa Amaan na hii leo timu ya JKU inaelekea kambini Tanzania bara, ambapo katibu wao Saadu Ujudi amesema kuwa Malale amesharejea rasmi JKU.

“ Kweli Malale amerejea kazini kwake JKU na leo asubuhi tulikuwa nae mazoezi na sisi tunajua karudi kazini kwake sasa Ndanda sijui vipi wao, kama wanamtaka Malale wafate taratibu na sheria mana hapa JKU ni kazini kwake lazima watufate sisi hapa ni kazini kwake , tukikubaliana tutawapa mana Yule ni muajiriwa wa Serikali.” alisema Saadu Ujudi katib wa JKU.

Kwa upande wao Ndanda FC tumezungumza na msemaji wao Idrissa Bandali, kuhusu kocha Malale ambapo alisema amerejea Zanzibar mara moja tu na hii leo atarejea kwenye mchezo kati ya Wagosi wa Kaya Coastal Union watakapowakaribisha Ndanda FC katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

“ Sitopenda kuzungumza sana kuhusu Malale lakini kocha wetu tumempa ruhusa mara moja kuelekea Zanzibar kisha kesho tutakuwa nae kwenye mchezo wetu.” alisema Bandali.

Nilimtafuta binafsi kocha huyo na kutaka kujua vipi yupo wapi JKU au Ndanda maana JKU wamesema hii leo wataondoka nae kwenda kambi Tanzania bara na Ndanda wanasema atakwenda Tanga na atakuwa kwenye bechi la ufundi.

Malale alichonijibu kuwa kwasasa haongei lolote na waandishi wa Habari kuhusu yeye kuwepo JKU au Ndanda FC.

“Kwa sasa niache sitopenda kuzungumza na waandishi wa Habari.” alisema Malale.

Inawezekana ikawa kuna wakati mgumu kwa kocha huyo ambapo JKU na Ndanda FC na zote zikimng’ang’ania kwa sasa, ambapo kwa upande wa JKU Malale ni muajiriwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Jeshi la kujenga uchumi, lakini Ndanda FC inaonekana kuwa na bonge la dau nono na pengine ni zuri zaidi, na hivyo kumfanya kocha huyo kuwa na wakati mgumu sana katika kipindi hiki maana Msemaji wa Ndanda FC, Bandali amesema “Sisi si watoto ni watu wazima hatuwezi kufanya mambo ya kitoto hatuwezi kumuharibia mtu kazi yake kisha hatujamuwekea mazingira mazuri, makubaliano yamefanyika kati yetu na yeye na ndio maana kakubali kuja kujiunga na Ndanda”.

Tanzania Yaendelea Kukwea Viwango Vya Ubora Wa Soka
Walichoamua Ukawa kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi wa Umeya Kinondoni, Temeke