Shirika la Afya Duniani – WHO, limetangaza kuwasilisha dozi milioni 18 za chanjo ya Malaria kwa Mataifa 12 ya barani Afrika, ifikapo mwaka 2025.
Mpango huo, utaendeshwa kwa usaidizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF, kama sehemu ya majaribio ya Mosquirix (RTS,S), iliyotengenezwa na kampuni kubwa ya dawa ya Uingereza GSK, na tayari imetolewa kwa zaidi ya watoto milioni 1.7 katika nchi tatu za Afrika ambazo ni Ghana, Kenya na Malawi.
WHO inasema majaribio hayo yamedhihirika kuwa salama na yenye ufanisi, na nchi hizo tatu zitaendelea kupokea dozi pamoja na nchi zingine tisa zitanufaika na mpango huo. Nazo ni Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Liberia, Niger, Sierra Leone na Uganda.
Mkuu wa WHO, Tedros Ghebreyesus amesema Malaria bado inasalia kuwa moja ya magonjwa hatari zaidi barani Afrika na huua karibu watoto nusu milioni kila mwaka, walio chini ya umri wa miaka mitano, ambapo mwaka 2021, asilimia 96 ya vifo vya malaria duniani vilitokea barani Afrika.