Matajiri wa mjini Manchester (Man City) usiku wa kuamkia leo walianza vizuri kampeni ya kusaka nafasi ya kucheza robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa kuifunga AS Monaco mabao matano kwa matatu.

Man City walitangulia kufungwa mabao mawili kwa moja dhidi ya wapinzani wao kutoka nchini Ufaransa, lakini juhudi za meneja Pep Guardiola na kikosi chake zilizaa matunda na kufikia malengo ya kuibuka na ushindi huo, ambao unawaweka katika mazingia ya kuendelea kupambana kwenye mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa baada ya majuma mawili mjini Monaco.

Man City walitangulia kufunga bao katika dakika ya 26 kupitia kwa mshambuliaji kutoka nchini England Raheem Sterling lakini AS Monaco walisawazisha kwa bao la Radamel Falcao dakika sita baadae na kisha Kylian Mbappe Lottin aliongeza la pili dakika ya 40.

Kipindi cha pili mshambuliaji Radamel Falcao alikosa mkwaju wa penati dakika ya 50 na kutoa mwanya kwa Man City kukusawazisha bao la pili kupitia kwa mshambuliaji wao kutoka Argentina Sergio Aguero dakika nane baadae.

Hata hivyo Falcao alisawazisha makosa yake kwa kufunga bao la tatu kwa AS Monaco dakika ya 61 kabla ya Sergio Aguero hajarejea tena nyavuni na kusawazisha dakika ya 71.

John Stones na Leroy Sane walifunga bao la nne na latano katika dakika ya 77 na 82 na kuiwezesha Man City kuibuka kidedea kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Etihad.

Katika mchezo wa mkondo wa Pili Man city watalazimika kulinda ushindi huo huku wakisaka ushindi zaidi dhidi ya wapinzani wao, huku AS Monaco watakua na lengo la kusaka mabao mawili kwa sifuri ama zaidi ili kujihakikishia nafasi ya kutinga robo fainali.

Diego Simeone: Tumefanikisha Lengo
Video: Maamuzi ya Mahakama kuhusu Mbowe