Kinda la Man Utd Axel Tuanzebe limesaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo, ikiwa ni siku kadhaa baada ya kuchezeshwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha wakubwa.

Tuanzebe mwenye umri wa miaka 19, alitumika kama mchezaji wa akiba wakati wa mchezo wa kombe la FA, ambapo Man Utd waliibuka na ushindi wa mabao manne kwa sifuri dhidi ya Wigan mwishoni mwa juma lililopita.

Mkataba wa mchezaji huyo  mzaliwa  wa  Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni wa miaka mitatu na utafikia kikomo mwaka 2020, huku taarifa za ndani ya klabu ya Man Utd zikieleza kuwa, huenda akaongozewa mkataba mwingine endapo ataendelea kufanya vizuri.

“Nilikua shabiki mkubwa wa Man Utd, lakini hii leo ni sehemu ya wachezaji wa klabu hii, ninafarijika sana.” Tuanzebe aliiambia tovuti ya Man Utd. “Kucheza kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wakubwa tena kwenye uwanja wa Old Trafford ilikua sehemu ya ndoto zangu, naamini hata familia yangu imefurahi.

“Nimekua ninajifunza mambo mapya kila kukicha, ninapata ujuzu kutoka kwa wachezaji wenzangu, ninatarajia kupata mengi zaidi kutoka kwa wachezaji wa kikosi cha wakubwa ambao nimeshacheza nao mara moja katika mchezo wa kombe la FA mwishoni mwa juma lililopita.”

Tuanzebe alisajiliwa na Man Utd mwaka 2013 katika kituo cha kulea na kuwaendeleza vijana cha klabu hiyo, na amekua akionyesha juhudi za kupambana.

Mino Raiola: Balotelli Ataamua Mwenyewe
FRAT Yakabidhi Kazi Kwa Haji Manara