Aliyekuwa Mwenyekiti wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Klabu ya Yanga, Yusuph Manji anatibiwa katika Hospitali ya Magereza ya Keko iliyopo jijini Dar es salaam kufuatia kukosa dhamana.

Hayo yamesemwa mapema hii leo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi, Huruma Shaidi wakati kesi yake na wenzake watatu iliposomwa hii leo.

Katuga amesema kuwa upelelezi bado haujakamilika hivyo ameiomba Mahakama kusogeza mbele kesi hiyo na ipangiwe tarehe nyingine, hivyo kesi hiyo imeahirishwa mpaka Agosti 4 mwaka huu.

Aidha, katika kesi hiyo ya Manji na wenzie watatu wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi Tanzania vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 pamoja na mihuri.

Hata hivyo, tangu wakamatwe na kusomewa mashtaka hayo, Washtakiwa hawakuruhusiwa kuongea chochote kwakuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Ulimi wamponza Peter Okoye, asakwa na polisi
JPM atoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vya mafuta nchini