Mapigano yanayoendelea kati ya makabila mawili ya Berti na Hawsa kwenye Jimbo la Blue Nile nchini Sudan, yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 33 huku familia nyingi zikiyambia makazi yao.
Wizara ya Afya nchini humo imesema watu 108 wamejeruhiwa katika ghasia hizo na maduka 16 yamechomwa moto tangu kuzuka kwa mapigano hayo Julai 11, 2022 yaliyosababishwa na mzozo wa ardhi kati ya makabila ya Berti na Hawsa.
Afisa wa mji wa Al-Roseires, Adel Agar amesema, “Tunahitaji wanajeshi zaidi ili kudhibiti hali hiyo, maana hali inazidi kuwa mbaya na watu wengi wameyakimbia makazi yao kuokoa masiha.”
Kulingana na Agar, amesema watu wengi walikuwa wanatafuta hifadhi katika vituo vya polisi na ghasia hizo zilisababisha vifo na majeruhi ambao binafsi hajajua idadi yake kwakua hana mamlaka kisheria kutoa taarifa.
Ingawa Agar hakutoa idadi ya vifo tofauti na Wizara iliyotyaja majeruhi lakini amesema wapatanishi walihitajika haraka ili kupunguza vurugu na matatizo zaidi.
Hata hivyo, tayari Serikali imepeleka Wanajeshi kudhibiti ghasia hizo na amri ya kutotoka nje usiku imewekwa na mamlaka kuanzia hapo jana Jumamosi Julai 16, 2022.
Naye Gavana wa Blue Nile, Ahmed al-Omda amezuia mikusanyiko yoyote au maandamano kwa mwezi mmoja ikiwa ni hatua ya kwanza katika kudhibiti hali hiyo.
Ghasia hizo zilizuka baada ya kabila la Berti kukataa ombi la Hawsa la kuunda mamlaka ya kiraia ya kusimamia upatikanaji wa ardhi, huku mwanachama maarufu wa Hawsa akisema juhudi za haraka zinahitajika ili kuondoa visasi.