Marekani imetishia kusitisha msaada wa awamu ya pili kutoka shirika la maendeleo la Milenia (MCC) iwapo Tanzania haitaumaliza haraka na kwa maridhiano mgogoro wa Zanzibar.

Taarifa toka chanzo cha kuaminika zimeeleza kuwa kiasi cha dola za kimarekani, milioni 472 (sawa na shilingi bilioni 999 za Tanzania) zilizotengwa kwa ajili ya Tanzania zimeshikiliwa hadi masharti waliyoyatoa yatekelezwe.

Pamoja na sharti la kumaliza mgogoro wa Zanzibar, Marekani pia imeitaka serikali ya Tanzania kutoa ufafanuzi/maelezo kuhusu watuhumiwa wa makosa ya mtandao hususani waliokamatwa katika kipindi cha uchaguzi mkuu.

Awali, Tanzania chini ya serikali ya awamu ya nne ilipokea kiasi cha dola milioni 698 (sawa na shilingi trilioni 1.46), hivyo kwa ujumla Tanzania inapaswa kupata trilioni 2.5 kutoka MCC. Kiasi hicho kitaifanya Tanzania kuwa nchi iliyopata fungu kubwa zaidi duniani kutoka MCC.

Hata hivyo, Katibu wa Hazina, Dk Servacius Likwelile alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu kuwepo kwa barua inayotoka MCC yenye maelekezo hayo, alisema kuwa bado hajaiona barua hiyo hivyo hawezi kueleza chochote.

“Tunawasiliana nao kwa mambo mengi, kwahiyo ni vigumu kueleza kama kuna barua yenye maelekezo hayo au la. Hadi nitakapoiona hiyo barua ndipo nitaweza kuzungumza lolote,” alisema Dk Likwelile.

Tofauti na ilivyo kwa misaada mingi, msaada wa MCC hutolewa kwa nchi wananchama bila kurejeshwa lakini moja kati ya masharti ya nchi zinazofaidika na misaada hiyo ni kuhakikisha inalinda utawala bora na demokrasia.

Balozi Seif: Dk Shein, Maalim Seif Wamekubaliana Uchaguzi Urudiwe
Ni Magufuli Kila Kona Ya Afrika Mashariki, #WhatWouldMagufuliDo itakuvunja Mbavu