Serikali imewaonya wauguzi wanaoweka kope bandia, kuvaa wigi na kushona nguo zinazobana kuendana na maumbo ya miili yao, kwani kufanya hivyo ni kukiuka utaratibu na miiko ya utoaji huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Rashid Mfaume katika mkutano wa wamiliki wa vituo binafsi vya afya na kuwataka kuhakikisha wanatoa taarifa za wagonjwa kulingana na mfumo wa serikali, utakaowezesha kupata taarifa kamili.
Amesema, “ni muhimu pia wauguzi kuzingatia miongozo ya kutoa huduma kulingana na taratibu za afya zinavyohitaji, utakuta muuguzi kaweka nyusi bandia machoni na mwingine nywele ndefu zenye rangi ya njano, au kuvaa nguo zilizobana.”
Dkt Mfaume amesema kuwa upo utaratibu wa sare za wauguzi pamoja na rangi na sio kuvaa kwa kujiamulia na kwamba kuna baadhi ya sare rangi zake haziruhusiwi, hata aina ya mishono pamoja na viwango vya kitambaa husika,ni lazima kuzingatiwa.
Aidha, ameongeza kuwa muonekano, tabia pamoja na mwasiliano na mteja upo utaratibu wa kuzingatiwa na katika kuhakikisha hilo linatimizwa, Muuguzi Mkuu atapita na kukagua.
Aidha, Dkt. Mfaume pia amewataka wenye vituo hivyo kutambua data hizo na kuzituma katika mfumo unaotakiwa kwa kuwa wanaongozwa na sheria pamoja na miongozo.
“Kwa mfano mwaka jana taarifa zineleza kuwa wanawake wajawazito waliojifungua katika vituo vya afya wanafikia 141,000 pekee idadi ambayo ni sawa na asilimia 62 peke yake,hivyo jambo la kujiuliza asilimia 38 walikwenda wapi,ambapo taarifa sahihi zingetolewa hali ingejulikana,” amesema.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Taasisi ya Benjamin Mkapa,Zawadi Dakika amesema vituo binafsi vina mchango mkubwa kwa uboreshaji wa afya nchini na kwamba ni muhimu kutekeleza yote yanayotakiwa.