Maseneta nchini Marekani wamesema kuwa wanaamini kuwa mwanamfalme, Mohammed bin Salman amehusika na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.
Msimamo huo wa Maseneta umekuja mara baada ya kufanya kikao cha siri na mkuu wa shirika la ujasusi la Marekani CIA, Gina Haspel.
Aidha, Seneta mwenye ushawishi mkubwa kutoka chama cha Republican, Lindsey Graham amesema kuwa ana imani kubwa kuwa Mohammed bin Salman (MBS) alipanga njama ya kumuua Khashoggi.
Khashoggi aliuawa ndani ya ofisi za ubalozi mdogo wa Saudi Arabia jijini Istanbul nchini Uturuki Oktoba 2. Mwanahabari huyo alikuwa ni mkosoaji mkubwa wa sera za Saudia hususani mwanamfalme bin Salman.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa CIA bi Haspel alikutana jana Jumanne na wajumbe wa Seneti wa Kamati ya Mambo ya Nje ambao hawakumung’unya maneno baada ya mkutano huo.