Utumiaji wa vifaa vya kupimia wagonjwa ambavyo vimeshakwisha muda wake huweza kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo muhusika kukosa kujiamini kutokana na kemikali zinazoweza kumpa mgonjwa madhara.
Hayo yamebainishwa na Dkt. Froliani Mwebesa kutoka Hospitali ya Rufaa Muhimbili hii leo Januari 13, 2023 wakati akizungumza na Dar24 Media na kuelezea madhara yatokanayo na matumizi ya vifaatiba vilivyokwisha muda wake.
Amesema, “Mara nyingi vifaa tiba ambavyo vinatumika kupimia watu, vinaweza kuwa na Chemical chochezi au vimelea ambavyo sio vinavyoweza kusababisha ugonjwa, na chemical hizi tunapozichanganya na vimelea ambavyo haviwezi kusababisha ugonjwa kwa wagojwa hapo ndipo tunapata majibu.’’
Aidha, Dkt. Mwebesa amefafanua kuwa, “kwahiyo kama mtu atakuwa ameathirika na ugonjwa au atakuwa na vimelea hivyo vyenye ugonjwa ndani yake tunapochanganya na zile chemikali pamoja na vimelea ambavyo haviwezi kusababisha ugonjwa basi tunaona kwa lugha ya picha.’’
Naye Izack Kimaro, mtaalamu wa Maabara amesema mara nyingi vifaa ambavyo vimkwisha muda wake haviruhusiwi kutumika kwa wagonjwa.
Ameongeza kuwa, “Kifaa kinaweza kutoa majibu ambayo sio sahihi, watengenezaji wanashauri kama kifaa kimekwisha muda wake kisitumike na watengenezaji wameandika katika bidhaa hiyo kwa maana hiyo anajua kwa muda fulani hakipaswi kutumika.’’
“wewe mwenyewe unapojua kuwa umetumia kitu ambacho sio sahihi unapoteza kujiamini na kusimamia kitu kama ni sahihi au sio sahihi kama kitu kimeisha muda wake kitolewe na kufanya kazi nyingine lakini sio kutibu wagonjwa”.