Mawaziri wa Nishati wa Tanzania, Rwanda na Burundi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mawaziri hao, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wamekutana na kufanya kikao na kukagua mradi wa umeme wa Rusumo, utakaozalisha megawati 80 na kila nchi kupata megawati 27.
Akizungumza na waandishi wa Habari Septemba 30, 2023 katika eneo la mradi, Wilayani Ngara Mkoa wa Kagera, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kukamilika kwa mradi huo kutapelekea ongezeko la umeme kwa nchi zote tatu na kuyaingiza Mataifa yote katika historia.
Amesema, “tumewasha mashine moja ya kuzalisha umeme na mashine mbili zilizobaki zitawashwa mwezi Oktoba mwaka 2023 tunawashukuru sana Marais wa nchi zote tatu kwa kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa pamoja Benki ya Dunia – WB na Benki ya Maendeleo Africa – AfDB, kwa kuchangia fedha zilizowezesha mradi huo kutekelezeka.”
Aidha, Dkt. Biteko ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na manufaa kwa nchi ikiwemo kuongeza megawati 27 katika gridi ya Taifa na kuimarisha upatikanaji wa umeme mikoa ya Kagera, Geita na Kigoma kitu ambacho kitachochea uwekezaji katika Viwanda na kukuza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kiujumla.