Mwanamuziki mahiri wa Bongo fleva, Mbwana Yusuf Kilungi maarufu Mbosso amefunguka juu ya kupambana na ugonjwa wa moyo, unaodaiwa kusababishwa na maumbile ya kuzaliwa.
Akizungumza na kipindi cha Fresh mwisho wa juma lililopita, Mbosso amesema amekuwa akipambana na ugonjwa huo kimya kimya na kuwajulisha watu wachache tu wa karibu yake.
Mbosso ameweka wazi kuwa wakati mwingine hupitia wakati mgumu kutokana na kuwa usingizi na wakati mwingine hupata maumivu ya mwili kupita kiasi.
“Ndiyo nina matatizo makubwa ya moyo lakini namshukuru Mungu naendelea vizuri, nafanya mazoezi ya viungo mara kwa mara ili kudhibiti hali hiyo lakini wakati mwingine napata shida hata kufanya mazoezi kwa vile nina maumivu,” amesema Mbosso.
Huku akibainisha kutopenda kuongelea chochote kuhusu masuala yake binafsi, lakini amesema tayari amewajulisha baadhi ya wanafamilia, watu wake wa karibu na mabosi wake akiwamo msanii Diamond Platnumz juu ya tatizo linalomsibu.
“Bosi wangu mmoja alikuwa anajua, mama yangu pia anafahamu hali hiyo na pia nilimjulisha Diamond pamoja na wazazi wenzangu ila binafsi huwa sizungumzii mambo yangu binafsi mara kwa mara,” aliongeza.
Aidha, Mbosso ameweka wazi kuwa daktari aliyemfanyia uchunguzi amebaini kuwepo kwa mafuta mengi mwilini kwake ambayo yameziba sehemu ya mishipa ya damu hali inayopelekea wakati mwingine kukumbwa na tatizo la kutetemeka.
Mwimbaji huyo amesema kwamba yuko tayari kusafiri kwa ajili ya matibabu ambayo ilikuwa ayafanye muda mrefu lakini alichagua kusubiri ili kuweka mambo sawa na kuiacha familia yake katika hali nzuri kwakuwa matibabu hayo yatachukua muda mrefu.
Ugonjwa anaougua Mbosso unajulikana kwa jina la Atherosclerosis, ukiwa ni wa hali ya kawaida ambao hutokea wakati dutu nata iitwayo plaque kujilimbikiza ndani ya mishipa na uundaji wa plaque huzuia mtiririko wa damu kuenea vizuri kwenye viungo vya mwili na tishu.
Maumivu ya kifua na upungufu wa kupumua ni dalili za kawaida za hali hiyo ambayo madaktari wanasema husababishwa na ulaji wa juu wa cholesterol, shinikizo la damu na kuvuta sigara.