Zikiwa zimebaki siku 4 kuifikia siku ya kihistoria kisiasa nchini (Oktoba 25), Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe ameweka wazi jinsi walivyojiandaa kuyapokea matokeo kile walichopanga baada ya matokeo ya uchaguzi Mkuu kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Mbowe aliuweka wazi mpango wa Ukawa baada ya kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa NLD, Dkt. Emmanuel Makaidi aliyezikwa katika makaburi ya Sinza, Dar es Salaam.

Akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua walivyojipanga kuyapokea matokeo, Mbowe alieleza kuwa umoja huo umepanga kuyakataa matokeo endapo sheria na taratibu za uchaguzi hazitafuatwa na haki kutotendeka, lakini wako tayari kuyapokea matokeo yoyote endapo haki na taratibu zote zitafuatwa kikamilifu.

“Kupokea matokeo ni mchakato ambao unaanzia katika hatua za kampeni, upigaji kura hadi wakati matokeo yanapotangazwa. Siwezi kusema eti tutakataa matokeo kwa sababu NEC watangaza tumeshindwa. Sio hivyo. Lakini tutapokea matokeo kama sheria, haki na taratibu nyingine zimezingatiwa mpaka kupatikana kwa matokeo,” alisema.

“Sisi Chadema na Ukawa tunaamini kuwa wananchi watamchagua rais wanaemuamini . lakini kama watawala watalazimisha kupindisha maamuzi ya wananchi kwa kutumia sanduku la kura, kamwe hatutakubali matokeo hayo. Na hapo amani tunayoihubiri inaweza kuwa ngumu kuidhibiti,” aliongeza.

Mbowe, wenyekiti wenza wa Ukawa pamoja na mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa jana waliungana na viongozi wengine wa vyama vya siasa na serikali kutoa heshima zao za mwisho kwa Dkt. Emmanuel Makaidi.

 

Maalim Seif Amtega Dkt. Shein Matokeo ya Urais
Mabomu Yakutwa Kwenye Gari La Mbunge Wa Chadema