Mahakama Kuu imetoa uamuzi wa kuwapa dhamana Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, leo mchana.
Jaji Rumanyika amesoma uamuzi huo ambao umewapa ushindi wanasiasa hao dhidi ya pingamizi lililokuwa limewekwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali kuzuia dhamana yao.
Mbowe na Matiko walikata rufaa Mahakama Kuu baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu wa kuwafutia dhamana kwa kutohudhuria mahakamani.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilisema kuwa imefikia uamuzi huo baada ya wawili hao kushindwa kufika Mahakamani kusikiliza kesi ya jinai inayowakabili bila sababu za msingi, wakiwa miongoni mwa viongozi saba wa Chadema.
Walikata rufaa Mahakama Kuu kupitia hati ya dharura sana, Novemba mwaka jana, lakini Mwendesha Mashtaka alikata rufaa pia Mahakama ya Rufaa akipinga Mahakama Kuu kusikiliza rufaa ya akina Mbowe akieleza kuwa ilikuwa kinyume cha sheria.
Hivi karibuni, Mahakama ya Rufaa iliamua Mahakama Kuu kuendelea kusikiliza rufaa hiyo ambapo leo wawili hao wamefanikiwa kurejea uraiani. Kesi dhidi yao inaendelea.