Mitihani inazidi kumkabili mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kumfungulia kesi yeye na mkewe, Dkt. Lilian Mtei.

Mbowe, mkewe Dkt. Mtui pamoja na Meneja wa Klabu ya Bilicanas, Steven Mlingo wameitwa mahakamani kupitia barua ya wito iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Ilala.

Mahakama imefanya uamuzi huo baada ya TRA kueleza kuwa imeshindwa kuwapata ili kuwapa hati ya wito mahakamani huku kesi hiyo iliyofunguliwa mwaka jana ikiwa imeshatajwa mara nne mahakamani hapo.

Washtakiwa hao waliofunguliwa kesi namba 402 ya mwaka 2016, wanakabiliwa na mashtaka matatu ikiwa ni pamoja na kutotumia mashine ya kielektroniki ya EFD kutoa risiti, kinyume cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015, kutoa nyaraka za uongo na kushindwa kutekeleza masharti ya sheria tajwa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo mwezi Mei mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Mke wa Mbowe, Dkt. Mtei ni daktari anayefanya kazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, lakini mwanasheria wa TRA, Marcel Busegano aliieleza mahakama hiyo kuwa walifika hospitalini hapo kumpa barua ya wito bila mafanikio.

Awali, Mbowe aliburuzana mahakamani na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) iliyokuwa ikieleza kuwa inamdai zaidi ya shilingi bilioni 1 ya kodi ya pango iliyokuwepo club ya Billicanas, sakata lililopelekea club hiyo ya usiku kubomolewa.

Maxwell Konadu Avishwa Viatu Vya Grant
Kala Jeremiah: Jina Harmorapa ni kubwa kuliko majina ya wasanii wenye albamu sokoni