Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kukamilisha utaratibu wa kuwapatia Hadhi Maalum Watanzania waishio nje ya nchi, yaani diaspora ifikapo mwaka 2024.
Hayo yamesemwa katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi kwa heshima ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba aliyepo nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 13 – 15 Novemba 2023.
Akifafanua masuala mbalimbali yaliyowasilishwa kupitia risala ya Watanzania iliyosomwa na Mwakilishi wa Umoja wa Watanzania waishio nchini Uholanzi, Bi. Sylvana Lubuva, Makamba alisema utekelezaji wa Hadhi Maalumu unategemea kufanyika kwa mapitio ya baadhi ya sheria za nchi kama ile ya ardhi na uhamiaji ili kurahisisha utekelezaji wenye tija kwa walengwa, yaani diaspora na kwamba mchakato huo unatajiwa kukamilika kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
“Miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele kwenye Hadhi Maalum ni haki ya kurithi au kurithishwa mali kwa diaspora wa Kitanzania aishiye nje ya nchi. Ili kutekeleza hili kuna maeneo ya sheria yetu lazima yabadilishwe ili watoto wenu wanaoishi huku nje waweze kurithi au kumiliki ardhi,” alisema Waziri Makamba.
“Sambamba na hilo, ni utaratibu wa kulipa visa pindi diaspora wa Tanzania wanaporudi nyumbani kwenye Hadhi Maalum, mtaruhusiwa kuja nyumbani na kukaa kwa muda mnaotaka bila malipo ya visa. Lakini kwanza ni lazima sheria yetu ya uhamiaji ipitiwe na kurekebishwa, ili kuruhusu kurudi nyumbani bila kulipishwa visa” alisisitiza Waziri Makamba.
Baadhi ya masuala mengine yatakayowanufaisha watumiaji wa Hadhi Maalum ni fursa na motisha mbalimbali za kuwekeza nchini Tanzania kupitia Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).
Kadhalika, Makamba alisisitiza umuhimu wa kujisajili kwenye mfumo wa Diaspora Digital Hub ambapo alisema licha ya kusaidia kuwatambua Watanzania waishio nje ya nchi, pia inarahisisha kwa kiasi kikubwa kuwarejesha nchini pindi majanga makubwa yanapotokea maeneo mbalimbali duniani.
Makamba yupo nchini Uholanzi kwa ziara ya kikazi ambapo siku ya pili ya ziara hiyo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uholanzi na kwa mujibu wa takwimu kutoka katika ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uholanzi, jumla ya watanzania wapatao elfu tatu (3,000) wanaishi nchini Uholanzi na maeneo ya karibu.