Mhubiri tata wa Kanisa la la Good News International la nchini Kenya, Paul Mackenzie, anadaiwa kuwa alitumia genge la wahalifu kuua wafuasi ‘waliokataa’ kufa hata baada ya kufunga kwa siku nyingi.
Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof. Kithure Kindiki ameyasema hayo na kuongeza kuwa genge hilo liliua kwa vifaa butu wafuasi wa Mackenzie waliochelewa kufa baada ya kufunga kwa siku kadhaa na wale waliojaribu kutoroka.
Waziri Kindiki ambaye alikuwa akiongea na Kamati teule ya Seneti inayochunguza vifo vya halaiki katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi, ameongeza kuwa Mackenzie alitumia mbinu mbalimbali kuficha mauaji hayo.
Amesema, “Alikuwa akitapeli wafuasi wake fedha lakini alipendelea kupewa hela taslimu badala ya kutumiwa kwa simu,na alitumia kanisa lake kushawishi wafuasi wake kuuza mali za na kisha kujiunga na kanisa, kisha baadaye, aliwahadaa akiwashawishi kutokula au kunywa hadi wafe ili wakutane na Yesu.”
Aidha, Prof. Kindiki amesema wale waliobadili nia na kutaka warudishwe nyumbani waliuawa na genge hilo, huku baadhi ya makaburi ya waathiriwa yakifunikwa kwa nyasi na ndiyo maana maafisa wa usalama wamekuwa na kibarua kigumu kuyatafuta.
Hadi kufikia sasa, tayari miili ya watu 241 imefukuliwa kutoka katika kipande cha ardhi ya ekari 800 inayoaminika kumilikiwa na Mackenzie na watu zaidi ya 90 wameokolewa.