Rais wa shirikisho la soka barani Ulaya (UEFA) Michel Platini amejiuzulu nafasi yake, baada ya kushindwa rufaa aliyokua ameiwasilisha kwenye mahakama ya kimichezo CAS iliopo nchini Uswis, kupinga maamuzi yaliyochukuliwa dhidi yake mwaka 2015.

Platini alisimamishwa na kamati ya maadili ya FIFA kabla ya kufungiwa kwa muda wa miaka sita kujishughulisha na soka sambamba na aliyekua rais wa shirikisho hilo la soka duniani, Sepp Blatter kufuatua tuhuma za kulipana pesa za kifisadi.

Mahakama ya kimichezo CAS, imechukua maamuzi ya kuiweka kapuni rufaa ya Platini na kuona kulikua na uhalali kwa kiongozi huyo kuadhibiwa na kamati ya maadili ya FIFA kufutia hukumu iliyomuweka hatiani.

Dakika chache baada ya hukumu ya rufaa yake kusomwa, Platini aliutangazia umma kupitia vyombo vya habari kwamba amejiuzulu nafasi yake ya urais wa UEFA.

Hata hivyo kiongozi huyo ambaye aliwahi kucheza soka akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa pamoja na baadhi ya klabu za barani Ulaya wakiwepo mabingwa wa soka nchini Italia (Juventus), amedai kutotendewa haki na mahakama hiyo kwa kusisitiza hakuhusiska katika makosa yaliyomuweka hatiani.

Platini mwenye umri wa miaka 60, alichaguliwa kuwa rais wa UEFA, Januari 26 mwaka 2007 na amekua madarakani kwa muda wa miaka minane mpaka alipoadhibiwa na kamati ya maadili ya FIFA mwaka 2015.

Uongozi Wa Leicester City Wakunwa Na Maamuzi Ya Riyad Mahrez
Serikali yagawa Sukari Buree!