Ni tukio lililoacha simanzi kwa familia, jamaa na mashabiki wa Mwanamuziki na mpiga Gitaa mkongwe wa Nchini DRC Dennis Lokassa maarufu kama Lokassa ya Mbongo ambaye siku ya kuzikwa kwake ikawadia jijini Kinshasa ikiwa ni miezi 10 tangu afariki.

Mazishi hayo yaliyotawaliwa na ukimya yalikuwa tofauti na mazishi ya awali ya Wanamuziki wenzake waliotangulia mbele za haki, huku Wanafamilia walijumuika na maafisa wa muungano wa muziki wa Kongo na baadhi ya wafanyakazi wenzake wa zamani.

Dennis Lokassa (Lokassa ya Mbongou).

Kiongozi wa muungano huo, Adios Alemba ambaye aliungana na Maitre John kuwasilisha ujumbe wa rambirambi kutoka kwa wasanii wenzake nchini DRC na kwingineko alisema kuutokuwepo kwa uhakika wa tarehe ya mazishi yake, tangu mwili wake uliposafirishwa kwa ndege kutoka Marekani hadi Kinshasa mwezi Aprili 2023 ambako alifariki, ndiyo sababu kuu ya wengi kutofika.

Ratiba ya maziko yake ilitolewa siku ya Jumatano Desemba 13, ikionesha Mwili wa Lokassa utazikwa Ijumaa Desemba 15, 2023 na hivyo muda kutoluwa rafiki kwa wapendwa walio mbali hasa nje ya nchi kuweza kufanikisha safari kuhudhuria maziko.

Lokasa akiwajibika enzi za uhai wake.

Siku ya Alhamisi Desemba 14, 2023 kulikuwa na mkesha katika chumba cha Joanny huko eneo la Matonge lililopo katika viungani vya jiji la Kinshasa na ratiba hiyo kuhitimishwa na ibada ya mazishi siku ya Ijumaa Desemba 15 katika Hospitali ya Du Cinquantenaire ambako mwili wake ulikuwa umelazwa hapo tangu Aprili.

Eneo alilozikwa Lokassa ni lile ambalo lipo nje kidogo ya jiji la Kinshasa ambapo baadhi ya Wanamuziki wengine mashuhuri kama vile Tabu Ley, Ndombe Opetum, La Poetre Lutumba Simaro, Tshala Muana, La General Defao Matumona na Mzee King Kester Emeneya walizikwa hapo.

Kutoka kushoto ni Dally Kimoko, Ngouma Lokito, Lokassa ya Mbongo, Yondo Kusala (Yondo Sister,) Zitany Neil, Shimita Lukombo (El – Diego) na Ballou Canta.

Mshirika wa karibu wa Lokassa kikazi Mwanamama Yondo Sister sambamba na Mpiga Besi mahiri Godess Lofombo walisema wamefarijika hatimaye kuona mwenzao amezikwa ikikumbukwa kwamba wote Lokassa na Yondo walifanya kazi pamoja katika bendi ya Tabu Ley ya Afrisa International na baadaye katika kundi la Soukous Stars.

Tangu kuondoka kwa Tabu Ley Afrisa International mwishoni mwa 1977, Lokassa alikuwa akiishi Abidjan, Ivory Coast na miji mingine ya Afrika Magharibi na pia aliweka makazi Ufaransa mwanzoni mwa miaka ya 1980 na baadaye kuhamia Marekani mwishoni mwa miaka ya 1990.

Kundi la Soukous Stars liliundwa na watu wanne ambao ni Lokassa ya Mbongou, Ballou Canta, Shimita el Diego na Dally Komoko, hiyo ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 1989-1990.

Baadhi ya nyimbo maarufu alizowahi kutunga Lokassa ni pamoja na Marie Jose, Bonne Annee, Monica, Sophia na Adiza kwa sehemu kubwa akimshirikisha katika uimbaji Mkongwe Shimita el Diedo na kundi la Soukous Stars.

Mazishi ya Lokassa yalikuwa marefu zaidi kuliko yale ya mpiga saksafoni, mtunzi na kiongozi wa bendi Kiamuangana Mateta Verckys aliyefariki Oktoba na kuzikwa Desemba 2022.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa wengi kutohudhuria mazishi ya Lokassa ni kufichwa kwa tarehe halisi ya kumpumzisha.

Ibada ya awali kwa Lokassa ilifanyika tarehe 1 Aprili katika Nyumba ya Mazishi ya Conner Healy na Kituo cha Kuchoma maiti huko Nashua, New Hamphshire. Marekani.

Hata hivyo, baadhi ya Wafanyakazi wenzake wa zamani kutoka Marekani kama vile Mekanisi Modero, Wawali Bonane na Ngouma Lokito walikuwa miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo.

Chanzo cha Maji Mto Ruvuma kutekeleza Mradi Chipingo - Mkaliwata
Serikali, AZAKI ziimarishe uhuru wa Habari, taarifa - TAMWA-ZNZ