Jeshi la Polisinchini Ugiriki, limesema miili ya wahamiaji wengine watatu imegundulika katika bahari ya magharibi ya Aegean, karibu na mahala ambako boti iliyojazwa wahamiaji kupita kiasi waliokuwa njiani kujaribu kuja barani Ulaya ilipozama.
Kugundulika kwa miili hiyo, kunafanya idadi ya waliokufa kwenye ajali hiyo kufikia watu 26 huku taarifa ya kikosi cha ulinzi wa pwani cha Ugiriki kikisema idadi ya manusura wa ajali hiyo hadi sasa inasalia kuwa 12, huku watu wengine 31 wakiwa hawajulikani walipo.
Hata hivyo,waliokufa ni pamoja na watoto watano na wawili kati ya manusura 12 wamekamatwa wakishukiwa kushirikiana na genge la wasafirishaji haramu wa binadamu, lililoandaa safari ya boti hiyo kutokea nchini Uturuki.
Aidha, manusura wa ajali hiyo, ambao wote ni wanaume walisema boti hiyo iliondoka karibu na eneo la Izmir lililopo upande wa magharibi mwa Uturuki ikiwa na watu 68, na ilipinduka kabla ya kuzama kwenye eneo la kina kirefu.