Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema katika mwaka 2022/2023, Serikali imesaini mikataba 31 yenye thamani ya shilingi bilioni 284.14 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji na kusisitiza juu ya matumizi bora ya chakula.

Majaliwa ameyasema hayo hii leo Aprili 5, 2023 Bungeni jijini Dodoma na kuongeza kuwa pamoja na changamoto za hali ya hewa, hali ya upatikanaji wa chakula cha kutosha katika maeneo yote nchini imeendelea kuimarika.

Amesema, “Mikataba hiyo inahusu ujenzi wa mabwawa nane, skimu mpya 13 na ukarabati wa skimu 17, hivyo kutaongeza eneo la umwagiliaji na kufikia hekta 778,210.6 kutoka hekta 727,280 mwaka 2021/2022.”

Aidha Majliwa ameongeza kuwa, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023, uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa ulikuwa tani milioni 17.4 ikilinganishwa na mahitaji halisi ya tani milioni 15.1 na kwamba uzalishaji huo umeihakikishia nchi utoshelevu wa chakula kwa asilimia 115 kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024.

Akizungumzia kuhusu maeneo yaliyokuwa na changamoto ya chakula Waziri Mkuu amesema hadi Januari, 2023, tani 29,084.21 za mahindi zilisambazwa katika Halmashauri 59 zilizokuwa na upungufu wa chakula kwa mwaka 2022/2023.

Amesema hadi kufikia Februari, 2023, upatikanaji wa mbolea umefikia tani 407,333 sawa na asilimia 58.33 ya mahitaji ya tani 698,260. Upatikanaji huo umechangiwa na tani 28,672 zilizozalishwa ndani, tani 251,697 zilizoingizwa , zikiwemo kutoka nje ya nchi na tani 126,963 ambazo ni bakaa ya msimu wa 2022/2023.

Aliyepona Marburg alia kuwapoteza ndugu, mama mzazi
Wajumbe 555 usimamizi maafa wapata mafunzo kuimarisha uwezo