Jumla ya watahiniwa 566, 840 watafanya mtihani wa kidato cha nne, unaotarajia kuanza kesho Jumatatu ya Novemba 14, 2022 katika shule za Tanzania Bara na Visiwani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Mitihani Taifa (NECTA), limesema kati ya wanafunzi hao watahiniwa 533,001 ni wa shule na 31, 839 wa kujitegemea ambapo watahiniwa kati ya hao wavulana ni 247,131 sawa na asilimia 46.19 na wasichana 287,870 sawa na asilimia 53.81.
Akiongea hii leo Novemba 13, 2022, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Athuman Amasi, amemezungumzia maandalizi ya mtihani huo na kusema katika idadi hiyo wapo watahiniwa wenye mahitaji maalumu 852 kati ya 480 wenye uoni hafifu, 62 wasioona, 19 wenye ulemavu wa kusikia, 152 wenye mtindio wa akili na 139 wana ulemavu wa viungo.
“Mwaka 2021 idadi ya watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 538,024 hivyo kuja ongezeko la jumla ya watahiniwa 28,816 sawa na asilimia 5.36 kwa mwaka 2022 ukilinganisha na mwaka 2021 na maandalizi ya mtihani huu wa kesho yamekamilika ikiwa ni pamoja kusambazwa kwa mtihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani katika mikoa ya Tanzania na Zanzibar.”
Hata hivyo, Amasi amesema mtihani wa kidato cha nne ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa sababu ina pima umahiri wa wanafunzi katika masomo yote aliyojifunza kwa muda wa miaka minne na kwamba matokeo ya mtihani huo yanatumika katika chaguzi za wanafunzi wanaojiunga na fani mbalimbali, Sekondari na elimu ya juu.