Serikali imempa Mkandarasi wa Kampuni ya Silo Power and Guangzhou Yidian Equipment LTD, inayojenga mradi wa Umeme Vijijini -REA awamu ya tatu mzunguko wa pili, ambao utafikia Vijiji 117 katika Wilaya ya Nzega, kuwalipa kwa Wafanyakazi wanaojenga mradi huo.
Agizo hilo, limetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga kwa Mkandarasi huyo baada ya kulalamikiwa na Wafanyakazi wake kuchelewesha mishahara hiyo huku Mbunge wa Bukene, Selemani Zedi naye akiwasilisha malalamiko Naibu Waziri Katika Kijijini cha Ikindwa kilichopo Kata ya Ikindwa Wilayani Nzega Mkoani.
Mbunge huyo alisema, “Mkandarasi huyu anakwamisha kazi kwa sababu amekuwa akichelewesha mishahara ya Wafanyakazi wake, na mpaka sasa hajawalipa kwa miezi kadhaa, naomba awalipe ili wafanye kazi kwa moyo ili mradi uishe kwa wakati.”
Akitoa agizo hilo, Naibu Waziri alisema Kampuni hiyo inatakiwa kuwalipa Wafanyakazi stahiki zao na kuongeza kuwa, “naagiza ndani ya siku saba, fedha za Vijana waliofanya kazi zilipwe, na kama unachukua Vijana kufanya kazi hakikisheni taratibu za malipo zimenyooka na walipwe fedha zao kwa wakati, na nitafuatilia.”
Tabora ina Vijiji 725, ambapo Vijiji 656 ambavyo ni sawa na asilimia 90.4 kati ya hivyo vimefikiwa na huduma ya Umeme, mara baada mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza na miradi iliyotekelezwa na TANESCO kukamilika, huku Vijiji vilivyobakia vikitarajia kufikiwa na Umeme ifikapo Desemba 30, 2023.