Mvutano kati ya Serikali ya mkoa wa Arusha na Mbunge wa Arusha Mjini, Golbles Lema umeendelea kuchukua sura mpya baada ya Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji hilo, Athmani Kihamia kudai mbunge huyo alitoa maneno ya kumdhalilisha mbele ya kadamnasi.

Akitoa malalamiko yake katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC) kilichohudhuriwa na Lema, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Meya wa Jiji hilo, Calist Lazaro,  Mkurugenzi huyo alidai kuwa Oktoba 19 mwaka huu katika kikao cha Kamati ya Mipango Mji, Lema alimdhalilisha kwa kudai ‘ameolewa na Mkuu wa Mkoa huyo’ ,  .

Alisema kuwa Lema alitoa kauli hiyo ya udhalilishaji dhidi yake baada ya kumwambia kuwa hawezi kutoa ufafanuzi na majibu ya masuali aliyouliza hadi apate ushauri kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Kufuatia madai hayo, Gambo alimhoji Mkurugenzi huyo kama ‘kweli yeye sio riziki’ na yeye alimjibu kuwa ni mwanaume lijari na anajua hakuna mwanaume anayepaswa kuolewa na mwanaume mwenzake.

Hata hivyo, Kihamia alieleza kuwa ameshamsamehe Lema na kwamba ingawa amekuwa akidhalilishwa mara kwa mara ataendelea kuvumilia ndio sababu hakuna ugomvi wa ngumi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti uligusia kwamba Meya amenitukana kule Musoma ni kweli na matusi mengine hayatamkiki, lakini nina uwezo wa kuvumilia matusi yao na ndio maana jiji linaendelea bila ngumi,” Kihamia anakaririwa.

Akizungumza katika mkutano huo bila kujikita katika malalamiko ya Mkurugenzi huyo, Lema alieleza kuwa watendaji wa wilaya hiyo wamekuwa wakishindwa kufanya maamuzi na kutekeleza makubaliano ya Baraza la Madiwani kwa kumuogopa Mkuu wa Mkoa.

Lema alidai kuwa hali hiyo ikiendelea, madiwani wa Chadema hawatashiriki katika vikao vyote vya madiwani hadi muafaka utakapopatikana.

Akijibu hoja ya Lema, Gambo alisema kuwa kutoshiriki vikao hivyo hakutakwamisha maendeleo ya jiji hilo kwani tayari bajeti ilishapitishwa na watendaji wanaweza kuendelea kutekeleza shughuli za maendeleo.

Alisisitiza kuwa mkoa huo uko shwari na utaendelea kuwa shwari, ”ukija kimjinimjini basi na sisi tatafanya mambo kimjinimjini na ukija kistaarabu tutamaliza mambo kistaarabu.”

Maalim Seif aona dalili za pingu mikononi mwake, 'SUK sio ya kuchezea’
Video: Mfalme wa Morocco kutua Dar na ndege sita kubwa