Mkutano wa kilele wa Viongozi wa Jumuiya ya kujihami ya NATO umekamilika mjini Brussels kwa jumuiya hiyo kuikemea China kwa kile wanachokitaja kuwa “sera za mabavu” pamoja na kuionya Urusi kwa matendo yake ya kichokozi.
Kupitia taarifa ya pamoja waliyoitoa baada ya mkutano huo wa siku moja, viongozi wa NATO wameelezea kwa matamshi makali wasiwasi wao juu ya tabia za China wanazosema zinakwenda kinyume na maadili ya jumuiya hiyo pamoja na sheria za Kimataifa.
Aidha, taarifa hiyo imeanisha kuwa malengo ya China na tabia ya taifa hilo la Kikomunisti ni changamoto kubwa linapokuja suala la ushirikiano duniani chini ya kanuni za kimataifa.
Mataifa wanachama wa Jumuiya hiyo wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuwa ni pamoja na kuimarika kwa uwezo wa kijeshi wa China, uhusiano kati ya nchi hiyo na Urusi pamoja na kile walichokitaja kuwa kukosekana uwazi mjini Beijing.
Kuhusu Urusi, wanachama wa NATO hususan mataifa ya Baltiki na nchi zinazopakana na Urusi zimesema bado zinaizingatia Moscow kuwa kitisho cha usalama.