Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ameitaka Mahakama Kuu nchini humo kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wake iliyofunguliwa na aliyekuwa mpinzani wake mkuu, Nelson Chamisa akieleza kuwa aliichafua mahakama.
Usikilizwaji wa kesi hiyo unarushwa moja kwa moja na kituo cha runinga cha ZBC.
Kupitia kiapo cha Mnangagwa kilichosomwa Mahakamani hapo leo, alisema kuwa Mahakama inapaswa kutosikiliza upande wa Chamisa kwani wakati wa kampeni walitoa kauli chafu dhidi ya mahakama na kufanya watu wakose imani na chombo hicho cha kutoa haki.
Mnangagwa ameeleza kuwa Chamisa alidai kwenye majukwaa kuwa Mahakama inapendelea upande wa chama tawala cha Zanu-PF. Pia, alidai kuwa Chamisa alikuwa anatoa ahadi zisizotekelezeka wakati wa uchaguzi.
Tume ya Uchaguzi na Mnangagwa wameitaka Mahakama kutupilia mbali madai ya Chamisa kwani yana makosa mengi ya kiufundi na kwamba yaliwasilishwa yakiwa yamecheleweshwa sana kiasi kwamba upande wa utetezi haukupata muda wa kutosha wa kuyapitia.
Katika hatua nyingine, Upande wa mlalamikaji umeeleza Mahakama kuwa Tume iliongeza idadi ya kura za Mnangagwa kwa kuhesabu mara mbili na kuweka kwenye majumuisho mara mbili (double counting).
Hata hivyo, Mahakama imeubana upande wa walalamikaji ikiwataka kuleta vielelezo vya ushahidi wa awali badala ya huu wa ziada. Upande wa mlalamikaji umedai kuwa haukuweza kuzishikilia kura zilizo kwenye masanduku kupata ushahidi huo na kwamba wamekatazwa kuwasilisha ushahidi kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta.
Endapo Mahakama itatupilia mbali mashtaka hayo, kwa mujibu wa sheria za Zimbabwe, Mnangagwa anaweza kuapishwa muda wowote baada ya saa 48.