Makamu wa Rais wa Zimbabwe aliyefukuzwa kazi, Emmerson Mnangagwa amemtaka Rais Robert Mugabe kuachia madaraka, huku akisema atarejea nchini humo iwapo atahakikishiwa usalama wake.
Ametoa wito huo na kusema kuwa anaungana na viongozi wa kijeshi pamoja na wanasiasa, wanaomtaka Rais Mugabe aheshimu maoni ya umma na kuondoka madarakani, ili nchi hiyo iweze kusonga mbele na kulinda hadhi yake.
Mnangagwa ambaye kwa sasa hayuko Zimbabwe amesema aliondoka nchini humo kwa sababu maisha yake yalikuwa hatarini baada ya kufukuzwa katika nafasi yake ya makamu wa Rais na Rais Mugabe.
Aidha, ameongeza kuwa Mugabe amemualika arejee nyumbani kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusu hali ya kisiasa ilivyo Zimbabwe, lakini amekataa wito huo hadi hapo atakapohakikishiwa usalama wake.
Hata hivyo, Jeshi la Zimbabwe lilisema Mnangagwa atarejea nchini humo hivi karibuni na amekuwa akiwasiliana na Mugabe ili waweze kukabiliana na hali ya sintofahamu iliyojitokeza kati yao.