Moto mkubwa ambao uliwaka katika jengo la bunge la Afrika Kusini mjini Cape Town ulizuka tena saa chache baada ya kusemekana kudhibitiwa.
Moto huo ulionekana kwanza ukitokea kwenye paa la jengo hilo siku ya Jumatatu, huku vikosi vya zima moto vikijaribu kuuzima moto huo.
Kwa mara ya kwanza moto huo ulizuka Jumapili na kuharibu kabisa chumba cha chini cha bunge hilo.
Mamlaka ilionya kuwa moto ungeweza kuongezeka kwasababu ya mazulia na sakafu ya mbao katika jengo hilo, huku msemaji wa bunge Moloto Mathapo aliiambia TimesLive ya Afrika Kusini kuwa baadhi ya wazima moto walifanya kazi usiku kucha kujaribu kuzuia moto zaidi.
Lakini waokoaji na watu wa zima moto 12 pekee ndio walikuwa kwenye eneo hilo wakati upepo ulipopamba moto juu ya Bunge la Kitaifa tena siku ya Jumatatu.
Taarifa kutoka kwa baraza la jiji iliyotoka saa nne za nchini humo ilisema kwamba ghorofa ya nne na ya tano ya jengo hilo ilikuwa imeharibiwa kabisa.
Waziri wa serikali Patricia de Lille alikiri kwamba kamera za CCTV hazikuwa zikifuatiliwa wakati moto wa kwanza ulipoanza.
De Lille alisema moto wa Jumapili ulisababisha kuteketezwa kabisa kwa bunge la Kitaifa na Maeneo mengine ya jengo la bunge – sehemu ambayo ni ya 1884 – pia yaliharibiwa vibaya.
Kwa sasa hakuna shughuli zinazoendelea katika jengo la bunge sababu wapo likizo, na hakuna aliyejeruhiwa.
Jengo hilo ni hifadhi kwa maelfu ya hazina vikiwemo vitabu vya kihistoria, picha na kazi muhimu za sanaa, ambazo maafisa walisema zimehifadhiwa.
Kumekuwa na wasiwasi kwamba ‘Keiskamma Tapestry’ ya thamani, ambayo ina urefu wa 120m (394ft) na inaandika historia ya Afrika Kusini, inaweza kuwa imeharibiwa.
Msemaji wa Bunge la Afrika kusini, Nosiviwe Mapisa aliliambia shirika la habari za Afrika Kusini kuwa haamini kama moto huo ulianza wenyewe.
Polisi wamemkamata mshukiwa ambaye atafikishwa mahakamani siku ya Jumanne kwa tuhuma za uchomaji moto, uvunjaji wa nyumba na wizi.