Mfanyabiashara maafuru ambaye pia ni kiongozi mkuu wa chama cha upinzani cha United Party for National Development, Hakainde Hichilema ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Zambia, akimshinda aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Edgar Lungu aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Patriotic Front.  

Mwanasiasa huyo amefanikiwa kushinda urais mwaka huu baada ya kugombea na kushindwa mara tano mfululizo, yaani 2006, 2008, 2011, 2015 na 2016.

Tume ya uchaguzi imetangaza kuwa Hichilema amepata kura 2,810,757 dhidi ya kura 1,814,201 za Edgar Lungu, katika majimbo 155 ya uchaguzi ambayo kura zimehesabiwa na kutangazwa kati ya majimbo 156 ya nchi hiyo.

“Hivyo, ninamtangaza Hakainde Hichilema kuwa Rais mteule wa Jamhuri ya Zambia,” Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia, Jaji Esau Chulu alitangaza kupitia Televisheni ya Taifa.

Tangazo hilo liliibua shangwe katika mitaa ya nchi hiyo, wafuasi wa chama kikuu cha upinzani wakifurahia ushindi huo.

Hichilema, amewahi kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya uhasibu kabla ya kuingia kwenye ulingo wa siasa.

Rais huyo mteule atakabiliwa na changamoto ya kubadili hali ya uchumi ya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hali ya maisha ya wananchi inapanda na kuiokoa thamani ya fedha inayoporomoka.

Hata hivyo, Edgar Lungu amepinga matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi akieleza kuwa kulikuwa na wizi wa kura.

Serikali yatoa idadi ya waliopata chanjo ya uviko 19
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Augusti 16, 2021