Serikali imesema hadi kufikia Agosti 14, 2021 jumla ya walengwa 207,391 wamepatiwa chanjo ya kukinga maambukizi ya corona ambapo takwimu hizo zinaonyesha wanaume wamechanjwa kwa asilimia 58.3 ambao idadi yao ni 121,002 na 86,389 wakiwa ni wanawake sawa na asilimia 41.7.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi ambapo amesema kuwa Serikali inaendelea kuratibu utoaji wa chanjo hiyo kupitia vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na binafsi 550 vilivyoidhinishwa hapa nchini.

Prof. Makubi amesema jumla ya dozi 1,008,400 za chanjo zilikuwa zimesambazwa katika mikoa yote 26 huku akisisitiza pasiwepo na sababu yoyote ya wananchi waliofika vituoni kukosa au kukataliwa kupata huduma ya chanjo.

“Tathimini ya utoaji chanjo tangu mikoa yote izindue, inaonesha mpaka kufikia jana jumla ya walengwa 207,391 wamepatiwa chanjo katika vituo vyote,”amesema Prof. Makubi.

“Natoa maelekezo kwa watoa huduma wote, kutumia dakika chache kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo kwa kila mteja atakaye mhudumiwa kwa magonjwa mengine ili kumpa nafasi ya uelewa na baadae yeye kuchukua maamuzi sahihi juu ya chanjo”amesema Prof. Makubi.

Rais Samia kushiriki mkutano wa SADC Malawi
Mpinzani ashinda urais Zambia, Lungu apinga matokeo