Boniface Gideon – Tanga.
Wakazi wa Vijiji Vitano kati ya tisa vilivyopo Kata ya Boma Wilayani Mkinga Mkoani Tanga, wamenufaika na Mradi wa utunzaji wa Rasilimali Bahari, unaosimamiwa na Shirika la Mwambao la Coastal Community Network Tanzania – CFMA, baada ya kukabidhiwa Boti kwa ajili ya kuongeza ulinzi shirikishi kwa jumuiya za usimamizi wa Rasilimali Bahari za na BMU.
Afisa Mtendaji Mkuu wa CFMA, Said Khalid amesema Boti hiyo yenye thamani ya Mil.35 imetolewa kwa Vijiji vya Boma kichakamiba, Mwaboza, Boma Subutuni, itasaidia kulinda Rasilimali Bahari na kuzuia uvuvi haramu, na imekabidhiwa ikiwa ni miezi michache baada ya Wavuvi na wakazi wa Vijiji hivyo kupatiwa Elimu ya Ufugaji wa miamba Bahari.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Kanali Maulid Surumbu amelishukuru Shirika Hilo na kuwataka Wadau mbalimbali kuendelea kuisaidia Jamii ya Mwambao wa Bahari, ili Matumizi ya Bahari yaweze kuleta matokeo chanya ya Kiuchumi kwa wakazi.
Amesema, ‘kwa niaba ya Wakazi wa Wilaya ya Mkinga tunatoa Shukrani Sana kwa msaada huu tunawaahidi kuwa msaada huu utatumika kama ilivyokusudiwa , niwaombe Wakazi wa Boma hususani Wavuvi nendeni mkaitumie Boti hii kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya za Usimamizi wa Rasilimali Bahari – CFMA (BMU), Wilaya ya Mkinga, Kassimu Khalfan amesema awali kabla ya kupokea msaada huo walikuwa wanatumia Mitumbwi na Majahazi kufanya doria za Ulinzi Baharini, Hali iliyowawia vigumu kuwapata wahalifu,
“Awali tulikuwa tunateseka Sana kufanya Ulinzi Baharini kutokana na kukosa Vifaa vya kisasa kwakuwa wahalifu Wengi wa Baharini wanatumia Boti za kisasa hivyo ilikuwa ni vigumu kuwakamata kirahisi lakini kwasasa tutawakamata kwa urahisi kwakuwa tunavifaa vya kisasa zaidi,” alisema Khalfan.