Msichana mwenye umri wa miaka 19, raia wa Uingereza aliyeutosa uraia wake mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 15 tu na kujiunga na kundi la kigaidi la Islamic State (IS), amezua gumzo baada ya kufungua shauri nchini humo akiomba arejeshewe uraia wake.
Shamima Begum, anadaiwa kujisalimisha kwenye kambi ya wakimbizi nchini Syria wiki mbili zilizopita, na wikendi iliyopita alijifungua mtoto wake wa kwanza katika kambi hiyo. Ameripotiwa kuukimbia mji wa Baghuz ambao ni ngome kubwa zaidi ya IS.
Msichana huyo kupitia kwa mwanasheria wa familia yake, ameiomba Serikali ya Uingereza kumruhusu kurejea nyumbani kama raia ili amlee mwanaye kwa utulivu. Begum aliiambia BBC kuwa hakuwahi kufikiria kujiunga na IS, lakini anachohitaji hivi sasa ni kuwa nyumbani.
Kwa mujibu wa BBC, Serikali ya Uingereza imepata baraka za kisheria za kumzuia msichana huyo kurejea nyumbani kama raia kwakuwa aliukana uraia wake.
Mwanasheria wa familia hiyo, Tasnime Akunjee amesema wamevunjwa moyo na uamuzi huo lakini wataendelea kutafuta msaada wa kisheria kuhakikisha binti huyo na mwanaye wanarejea nyumbani.
Sheria ya Utaifa ya Uingereza ya Mwaka 1981, inampa mamlaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kumnyima mtu uraia ikiwa atajiridhisha kuwa ni kwa faida ya umma na kwamba uamuzi huo haumfanyi mtu huyo kukosa taifa ambalo atakuwa raia wake.