Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Segerea, Julius Mtatiro amekosoa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuwaweka rumande maafisa ardhi waliochelewa kufika katika eneo la kazi akidai kuwa ilikuwa kinyume cha sheria.

Mkuu huyo wa wilaya ya Kinondoni alitoa amri iliyotekelezwa ya kuwaweka selo maafisa ardhi waliochelewa kufika katika eneo la kazi walilokubaliana awali.

Jana, Maafisa hao walikubaliana na Makonda kufika katika eneo la Nakasangwe, Kata ya Wazo  mapema asubuhi ili kujadili kuhusu mgogoro wa ardhi lakini walifika majira ya saa tano, ndipo alipoamuru wakamatwe na kuwekwa katika kituo cha polisi Kawe kwa saa 6.

Mtatiro

Kupitia Facebook, Mtatiro ameandika:

“Nilipo- post juu ya jambo hilo mjadala mkubwa wa wananchi umekuwa ni kutaka kujua sheria inaelekeza nini kwa mamlaka ya wakuu wa wilaya. Kwa uelewa wangu wa shahada ya kwanza ya sheria nimeona niwawekee hapa ufafanuzi wa kisheria kwa ajili ya faida yenu na mjadala mwingine tena.

 

SHERIA INASEMAJE?

Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 (The Regional Administration Act) kwenye kifungu cha 15 (1) imeweka sharti muhimu kwa Mkuu wa Wilaya ikiwa atahitaji kutumia mamlaka ya kuamrisha mtu akamatwe, kifungu hicho kinamtaka afanye hivyo pale tu ambapo atakuwa amejihakikishia kuwa kosa lililotendwa na mhusika athari yake huwa ni kukamatwa na kushtakiwa na tena sheria imeweka masharti ya namna ya kushtaki.

JE KISHERIA DC MAKONDA ANA HAKI YA KUWAWEKA NDANI WATAALAM HAO?

Hapana, kisheria hana mamlaka hayo, Kosa walilotenda watalaam hawa wa ardhi ni la kuchelewa kwenye eneo la kazi, kosa la kuchelewa mahali kwenye majukumu ya kawaida ya kupima ardhi haliwezi kamwe kumfanya mtu ashitakiwe hadi pale ambapo kuchelewa huko kutakuwa kumesababisha madhara makubwa na yanayoweza kuthibitishwa mahakamani. Kwa hiyo kama Makonda amewaweka ndani anawajibika kwa mujibu wa sheria hii kuwapandisha kizimbani haraka kesho (Jambo ambalo atalikwepa kwani hawana kosa ambalo lina “amount to being arrested and tried” yaani “kukamatwa na kushtakiwa”).

JE, MAKONDA AKISHTAKIWA ANAWEZA KUPEWA ADHABU GANI?

 Bahati nzuri, sheria hiyohiyo katika kifungu cha 15 (1) imeeleza kuwa ikiwa mkuu wa wilaya atatumia mamlaka yaliyowekwa na kifungu husika kwa maana ya kutumia madaraka yake vibaya, atakuwa ametenda kosa na anaweza kushtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 96 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code).

Kifungu hicho cha 96 (1) na (2) kinaeleza kuwa Mtu yeyote ambaye ameajiriwa kwenye utumishi wa umma (akiwemo Mkuu wa Wilaya) anayetenda au kuamrisha utendekaji wa jambo kwa kutumia vibaya madaraka ya kazi yake, kitendo chochote cha dhuluma ambacho kinazuia haki ya mwingine atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani anaweza kufungwa miaka mitatu jela.

JE WATAALAM HAO WA ARDHI WANAWEZA KUMSHITAKI MAKONDA?

 Ndiyo, wataalam wa Ardhi waliotendewa amri hiyo wanaweza kumshitaki Paul Makonda kwa kitendo chake cha kutumia vibaya madaraka yake lakini bahati mbaya itakayowakuta ni kwamba Sheria hiyo hiyo ya Kanuni ya adhabu kwenye kifungu cha 96 (3) imeweka sharti lingine kuwa Uendeshaji wa shitaka kwa husika hautaanzishwa mpaka kitakapotolewa kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (Kesi ya Nyani amekabidhiwa ngedere).”

Viongozi waliowahi kuiba mali za Umma wajisalimisha kwa Rais
Alichokisema Papa Francis Baada ya Kutua Kenya