Mtoto wa miaka mitatu, Sungwa Kulwa mkazi wa Kishapu mkoani Shinyanga, amefariki dunia baada ya kushambuliwa na fisi wakati akicheza na watoto nje ya nyumba yao.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo lilitokea Aprili 30 mwaka huu saa moja jioni baada ya mnyama huyo kutoka vichakani ghafla na kumshambulia mtoto.

Amesema baada ya fisi huyo kuwatokea alimshambulia Kulwa na kumburuza umbali wa mita 100 na kumwachia baada ya kusikia kelele za wananchi waliokuwa wanamfukuza.

ACP Debora amesema baada ya tukio hilo kuripotiwa idara ya wanyama pori halmashauri ya wilaya ya Kishapu ilifika na kutoa elimu ya kujikinga na wanyama hao na kutoa taarifa mapema wanyama wakali wanapotokea.

Aidha ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wako katika mazingira salama muda wote wasiachwe pekeyao hasa kipindi hiki ambacho fisi wamekuwa wakionekana maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Uhispania yaruhusu watu kutoka nje kwa mara ya kwanza
Dkt. Nchemba ateuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria