Mtuhumiwa aliye unganishia bomba la mafuta nyumbani kwake, Samwel Kilanglani (63) ametambulika kuwa ni mfanyakazi mstaafu wa bomba la kusafirisha mafuta Tanzania na Zambia (Tazama).
Hivyo Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko amesema anaandaa ripoti kuhusu tukio hilo na ataitoa saa tisa leo, Jumanne.
“Hili ni suala kubwa linalohusu uchumi wa nchi. Ni sawa na mtu kuvamia kambi ya jeshi.” amesema Deusdedit
Kamanda wa kikosi cha Polisi Bandari Roberty Mayalla amesema mtuhumiwa huyo alijiunganishia bomba kwa utaalamu wa hali ya juu kipindi mabomba hayo yanajengwa.
Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika naye amesema mtuhumiwa huyo alijiunganishia bomba la TPA kwa njia ya kuchomelea na kuunganisha moja kwa moja kwenye mantaki yake mawili yaliyochimbiwa chini ndani ya nyumba yake na kupelekea mafuta yanayopelekwa sehemu husika hayafiki kama yalivyokusudiwa.
“Mafuta yanaweza yakapelekwa lita 4,000 sehemu husika lakini hayafiki yote mengine yanaenda kwa mtuhumiwa huyu matokeo yake wanajiuliza haya mengine yameenda wapi,” amesema Kitalika.
Kilanglani anatuhumiwa kutoboa bomba la mafuta ya dizeli la Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kuliunganisha kwenye mantaki mawili ndani ya nyumba yake iliyopo Tungi Kigamboni.