Hatimaye Kiungo kutoka DR Congo Mukoko Tonombe amafunguka sababu ya kilichomfanya amwage machozi baada ya kuifungia Young Africans kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting juzi Jumanne (Novemba 02), Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kiungo huyo ambaye alianza kwa mara ya kwanza kikosi cha kwanza cha Young Africans kwenye mchezo wa juzi Jumanne, amesema kabla ya kupata nafasi ya kurejea kikosini alipitia changamoto kadhaa ambazo aliamini huenda zingemkwamisha katika soka lake.

Amesema alikua anatafakari bila kupata majibu, lakini alijipa moyo na kuamini ipo siku mambo yatakwisha na maisha yake ya furaha yatarudi.

“Nimekuwa nikipitia wakati mgumu, msimu uliopita baada ya kupata kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Simba mambo yamekuwa sio mazuri kwa maisha yangu ya soka,” amesema Mukoko na kuongeza

“Kuna wakati nilijikuta nakata tamaa na kulia nikiwa peke yangu kambini na nyumbani ndio maana baada ya kufunga nilijikuta nalia kwa furaha iliyochanganyikana na uchungu.”

“Niwashukuru mashabiki wote wa Yanga walioonyesha kuwa nami katika kipindi chote kigumu. Nawaahidi kuwapa raha zaidi.”

Mukoko alikosa michezo mitatu ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu, kufuatia kadi nyekundu aliyooneshwa kwenye mchezo wa Fainali wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba SC mjini Kigoma, kwa kumpiga kiwiko John Raphael Bocco.

Pia usajili wa wachezaji Yanick Bangala na Khalid Aucho umekua changamoto kubwa sana kwa Mukoko , hali ambayo imemfanya apoteze nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Young Africans.

Tory Lanes ategemee Mvua ya miaka 23 Jela kwa kumpiga Risasi Megan Thee
Jay Z aifuta tena account yake ya Instagram